‘Komasava Remix’ kati ya Diamond na Jason Derulo iligharimu Ksh.24 milioni - meneja wa Diamond SK Sallam

Chley na Khalil pia wanashiriki kwenye ‘Komasava Remix’ pamoja na wakali hao wawili.

Muhtasari

•Meneja SK Sallam alidai kuwa 'kushoot' video hio ilifanyika katika nchi kadhaa ikiwemo Dubai,Paris.

•Hadi sasa  wimbo huo umefikisha  'views' zaidi ya milioni 3.5  kwenye YouTube.

Jason Derulo pamoja na Diamond platnumz
Image: screengrab

Wimbo wa Komasava remix wake  Diamond Platnumz aliyemshirikisha mwimbaji nyota wa muziki wa RnB kutoka Marekani, Jason Derulo uligharimu angalau KSh.24 milioni.

Video ya wimbo huo ilifanyika  katika nchi kadhaa ikiwemo Dubai  ambapo Diamond na Jason Derulo  waliungana.

Akifafanua gharama, meneja wa muda mrefu wa Diamond SK Sallam amefichua kuwa bajeti ya wimbo huo ni kubwa zaidi ya Tsh500 milioni (Sh24 milioni) ikiwa kila matumizi yatazingatiwa kuanzia vifaa, eneo, uzalishaji, malazi na mambo mengine.

"Video ilipigwa katika maeneo tofauti na waongozaji watatu tofauti wa video. Kuna tukio la 'dessert scene' lililopigwa huko Dubai, tukio lililopigwa huko Paris, na tukio ambalo linaangazia Diamond na Jason lilifanyika katika eneo tofauti huko Dubai pia," SK Sallam alisema.

Kutokana na mienendo hiyo, Sallam anasema walilazimika kutumia fedha nyingi kufadhili mradi huo kwani 'kushoot'  kulihusisha watu kadhaa wakiwa sehemu ya wafanyakazi.

Diamond pia alilazimika kusafiri kwa ndege hadi Dubai na waimbaji wawili wa Amapiano wa Afrika Kusini Chley Nkosi, Khalil Hilson, na timu yao,  huku akiwahudumia malazi pamoja na gharama nyinginezo.

Chley na Khalil pia wanashiriki kwenye ‘Komasava Remix’ pamoja na wakali hao wawili.

Hata hivyo, Sallam ambaye anamiliki kituo cha redio pinzani cha Mjini FM cha Wasafi FM ya Diamond, anasema kilicholeta changamoto kubwa ya mradi huo, ni kurusha matukio huko Dubai.

“Haikuwa rahisi kuweka kila kitu pamoja kwa sababu hapakuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa vyema. Tulipewa hati ya mwisho ya siku mbili kukamilisha malipo ya ada za ushirikiano (na timu ya Derulo), malipo ya maeneo yaliyotumiwa, na malipo ya vibali vya 'kushoot'  kwenye maeneo.'

Aliongeza;

'Pia kulikuwa na gharama za kuweka usanidi uliotumika katika maeneo tofauti kati ya maelezo mengine. Kusema kweli, ikiwa tutazingatia kila gharama bajeti iko juu zaidi,’

Kufikia wakati wa uchapishaji huu, wimbo wa video uliotolewa siku tatu zilizopita, hadi sasa umefikisha  ' views' zaidi ya  milioni  3.5  kwenye YouTube.