Kundi la wanamuziki ndugu, PSquare linaendelea kushuhudia nyufa zaidi kutokana na msururu wa kutoelewana baina ya ndugu hao mapacha.
Katika kile kinachoendelea, Peter Okoye maarufu kama Mr P amemuandikia barua pacha wake, Paul Okoye maarufu kama Rudeboy, akimtuhumu kuhusika katika masaibu na mamlaka ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria, EFCC.
Mr P katika barua hiyo anasisitiza kwamba yeye hana ushindani wowote na pacha wake, akisema shinda yake na kakake ni kuona jinsi anamchafulia jina kwenye msururu wa mahojiano kadhaa ambayo amekuwa akifanya.
“Ndugu yangu mpendwa, kama ambavyo nimekuwa nikikwambia mara kadhaa, siko katika ushindani na wewe au mtu yeyote yule. Hata hivyo, kukuona ukifanya mahojiano kadhaa ukipuuzilia mbali juhudi zangu katika kundi ambalo sote tulianzisha na kujenga pamoja inazungumza mengi,” alisema.
Mr P alisema kwamba hajafurahia na tetesi kutoka kwa pacha wake kwamba yeye (Rudeboy) ndiye alikuwa anahusika kaitka utunzi wa 99% ya ngoma za PSquare huku akisema kuwa ngoma ambayo yeye (Mr P) alitunga ilibuma.
Mr P alilalama kwamba pacha wake anamchukulia poa wakati yeye katika kila mahojiano anafanya huwa anazungumzia ‘sisi’ na wala si ‘mimi’ kwa kurejelea kundi la PSquare.
Alimkumbusha pacha wake katika barua hiyo kwamba wao wote sio wasanii wenye talanta zaidi duniani bali kilichowavutia mashabiki kwao ni juhudi za pamoja ambazo walikuwa wanaweka kama kundi la PSquare.
Pia, Mr P alimtuhumu kaka yao mkubwa, Jude kwa kuungana na pacha wake ili kujinufaisha kutokana na mafao ya kundi la PSquare badala ya kuungana naye ili watie juhudi za kurudisha jina lao kaitka nambari ya 1 kwenye chati za muziki wa Afrobeats.
“Badala ya kuungama na mimi ili kurudisha namba yetu ya 1, uliamua kuungana na Jude ili kuchukua nambari moja kwenye kundi la PSquare, kila mara kutafuta fursa ya kunitenga na kuninyanyasa,” alilalama.
Alimalizia akimwambia pacha wake kwamba badala ya kujidai kuwa nyuma ya 99% ya ufanisi wa PSquare, yeye kama Mr P amempa haki ya kuchukua 100% ya ufanisi wa kundi hilo.