Mchekeshaji MCA Tricky amefichua kwamba wazazi wake walikuja kufahamu kwamba huwa anaonekana kwenye runinga akichekesha watu baada ya muda.
Akizungumza na Oga Obinna, Tricky alisema kwamba iliwachukua wazazi wake muda wa mwaka mmoja kujua kwamba ni mwanao amekuwa akichekesha watu kwenye runinga.
Akiulizwa kwa nini iliwachukua muda mrefu hivyo, Tricky alikiri kwamba hawakuwa na uwezo wa kumiliki runinga lakini pia hawangeamini kwamba mwanao ndiye alikuwa anaonekana kwenye runinga.
Mchekeshaji huyo alisema wakati anaanza kuchekesha kwenye Churchill Show akivaa kama chokoraa, alikuwa ni mwanafunzi wa chuo katika mwaka wake wa 2, hivyo wazazi hawangeamini kuona mwanao akiwa kama chokoraa kwenye runinga hali ya kuwa wanajua yuko chuoni KU.
“Wazazi wangu walikuja kujua kwamba niko kwa runinga baada ya mwaka mmoja. Jambo la kwanza hawakuwa na TV na la pili ni kwamba yule Tricky aliyekuwa kwenye TV hakuwa mwanao. Hawangeamini ni mimi kwa sababu kwenye TV nilikuwa mtu Fulani tofauti,” alisema.
Tricky alifichua kwamba suala la wazazi kukosa TV lilimsaidia kwa kiasi Fulani hadi pale mjomba wake alipokuja kugundua na kusambaza ujumbe kwa familia.
“Mjomba wangu ndiye aligundua niko kwa TV na akanipa onyo nichunge watu wa TV wasinimalizie pesa akidhani mimi ndio nilikuwa nalipa ili kuchekesha watu jukwaani,” alifichua.