Rapa anayejinadi kama nambari
moja wa Kenya kwa muda wote, Khaligraph Jones amedokeza kuwa ujenzi wa jumba
lake la kifahari ambazo limezua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii huenda
ulichochewa na maisha ya kifahari ya rapa kutoka Marekani, Rick Ross.
Jones alichapisha video
kwenye Instagram yake akionyesha ukubwa, upana na umaridadi wa jumba hilo na
kusema kwamba wengi wa watu ambao wanakejeli muundo na ujenzi huo ni wale ambao
hawajazea kuona mijengo ya kibinafsi kama hiyo.
Msanii huyo alisema kuwa
kwa jinsi ameboresha mazingira ya jumba hilo la kifahari, watu wanaokwenda kule
watapata kuhisi uwepo kama ule wa boma la Rick Ross.
“Hamjazoea hizi
settings, hapa ukikuja ni kama umeingia Amerika, kwa Rick Ross. Heshima ni
lazima kwa OG,” Khaligraph Jones alisema huku akicheka.
Siku ya Jumatatu, Jones
alishangazwa na watu ambao walikuwa wanachapisha picha na video za jumba lake
mitandaoni wakiambatanisha na kauli za dharau kuhusu mjengo huo.
Hata hivyo, alionyesha
kutoshtushwa na kauli hizo hasi akisema kwamba habari za kusemwa kuhusu
mafanikio yake ndizo habari ambazo alikuwa akiomba kwa muda mrefu.
"Unaamka unapata unatrend sababu
umejenga nyumba kubwa inakaa kama maduka, Mungu anajua haya ndio matatizo
niliyokuwa natamani," Khaligraph alisema.
Jones amekuwa akionyesha maendeleo ya
ujenzi wa jumba hilo ambalo liko viungani mwa Ngong tangu lilipoanza.
Wengi wamekuwa wakimsuta kwa ujenzi huo
wanaoufananisha kama duka la jumla, wengine wakiutaja kama mjengo wenye mfanano
wa chuo kikuu, lakini yeye amesimamia kauli yake kwamba ni boma lake la kuishi
wala si la kufanya biashara.