Rapa mahiri wa Kenya Brian Omollo almaarufu Khaligraph Jones ameungana na wanamtandao wengine kuifanyia mzaha nyumba yake kutokana na ukubwa wake.
Siku ya Jumanne asubuhi, mwimbaji huyo wa kibao ‘Yes Bana’ alionyesha picha yake akiwa amekaa kwenye kochi kubwa kwenye sebule ya jumba lake kubwa la kifahari.
Kwenye sehemu ya maelezo ya chapisho hilo, alitangaza kwa kejeli kwamba alikuwa katika maduka ya Garden City na kubainisha kwamba alikuwa tayari kusikiliza ushauri.
“Habari ya asubuhi Kenya, ninaripoti moja kwa moja kutoka Garden City. Niko tayari kwa ushauri wako wa kuanza siku yangu, OG itaheshimiwa,” alisema.
Siku ya Jumatatu, mwimbaji huyo aliibu kwa kejeli baada ya kundi la wakosoaji kukejeli jumba la kifahari ambalo alimalizia kulijenga hivi majuzi.
Katika siku mbili zilizopita, wakosoaji kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakikejeli jumba kubwa la kifahari ambalo rapa huyo alijenga huku wengine wakilinganisha na jumba la mall.
Katika majibu yake, Khaligraph alionekana kuwacheka wakosoaji
hao huku akibainisha kwamba hayo ndiyo aina ya matatizo aliyoyataka.
"Unaamka unapata unatrend sababu umejenga nyumba kubwa inakaa kama maduka, Mungu anajua haya ndio matatizo niliyokuwa natamani," Khaligraph alisema.
Rapa huyo mahiri amekuwa akitrend haswa kwenye mtandao wa kijamii wa X asubuhi ya Jumatatu kwa sababu ya nyumba yake.
Picha ya Khaligraph na mama yake wakiwa wametulia ndani ya jumba hilo kubwa iliwekwa kwenye mtandao wa X Jumapili jioni kabla ya mwanamtandao mmoja kuihariri na kuifanya kuonekana kama duka.
Wanamtandao wengine wengi walichukua picha iliyohaririwa na kuitumia kufanyia mzaha jumba hilo.