Abba Marcus, mtoto wa mwimbaji nguli wa Uganda Joseph Mayanja almaarufu Chameleone ametoa ombi la usaidizi kwa baba yake ambaye anasema anapambana na matatizo makubwa ya kiafya.
Katika video ambayo alichapisha kwenye mitandao ya kijamii, Abba alifichua kuwa babake anaugua ugonjwa wa kongosho ambao umesababishwa na unywaji pombe kupita kiasi kwa muda mrefu.
Kijana
huyo alisema kwamba babake amepambana na uraibu wa pombe kwa muda mrefu ambao
umeleta matatizo makubwa ya kiafya ambayo madaktari wanasema yanaweza kumuua
ikiwa hataacha kunywa.
"Baba
yangu anaugua ugonjwa mkali wa kongosho. Mara nyingi hii ni hali husababishwa
na matumizi ya mara kwa mara ya pombe. Katika kesi hii, hiki ndicho hasa
kinachoendelea na baba yangu. Ili kuweka mambo kwa urahisi, baba yangu
anapambana na uraibu wa kileo. Hiki ni kitu ambacho amekuwa akiteseka nacho kwa
muda mrefu sasa,” Marcus alisema.
Mwanawe Chameleone alithibitisha kuwa mwimbaji huyo bado anapokea matibabu hospitalini baada ya kulazwa wiki iliyopita akiwa katika hali mbaya sana.
Pia alifichua kuwa madaktari tayari wamemwonya babake kuhusu uraibu wake wa pombe wakimtahadharisha kwamba hana muda mwingi wa kuishi ikiwa ataendelea kupenda chupa.
“Nataka mfahamu kwamba baba yangu akiendelea na mtindo huu, kwa mujibu wa madaktari amebakiza miaka miwili ya kuishi. Hii inanivunja moyo sana kwa sababu huyu ni baba yangu, nimemfahamu katika maisha yangu yote, namfahamu zaidi mtu yeyote duniani, hata watu wanaosikiliza muziki wake,” alisema.
Kufuatia hayo, Abba alitoa wito kwa watu wanaojali msanii huyo mahiri, wakiwemo mashabiki wake kumsaidia kukabiliana na uraibu wake wa pombe.
Wakati huo huo, aliwakosoa babu na nyanya yake, marafiki wa Chameleone na mapromota wa muziki wa Uganda waliompangia shoo akidai kuwa hawamjali mwimbaji huyo hata kidogo ila wanajali tu thamani ya dhamani yake ya kifedha.
Abba pia alikanusha madai kwamba mama yake, Daniella Atim, ndiye aliyesababisha masaibu ya kiafya ambayo mwimbaji huyo anapambana nayo.
Mama huyo wa watoto watatu kwa sasa hayuko tena na mwimbaji huyo mkongwe kwani waliachana miaka michache iliyopita.