Staa wa filamu Art Evans aliyefahamika kwa kucheza filamu ikiwemo Die Hard 2, The X-Files na Everybody hates Chris ameaga dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari.
Kifo cha mwanafilamu huyo kilichotukia mnamo Jumamosi kilidhibitishwa na wakala wake aliyesema kwamba Evans aliaga dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari.
Arthur James Evans aliyefahamika kama Leslie Barnes kwenye filamu ya Die Hard 2, alizaliwa katika mtaa wa Berkeley kwenye jimbo la California, mnamo Machi 22, 1942.
Mbali ya kushiriki katika filamu za Die Hard 2 na The X-Files, mwanafilamu huyo pia alihusika katika filamu nyingine na vip[indi vya televisheni katika miaka ya kati 1970s na 1990s.
Baadhi ya vipindi vya runinga alivyohusishwa ni ikiwemo M*A*S*H iliyochezwa kati ya mwaka 1972 na 1983 ijapokuwa alihusika katika kipindi kimoja akiitwa Dolan.
Pia alishirikishwa katika shoo ya televisheni ya Hill Street Blues, 9 to 5, Sister and Amazing Grace, Walker na Texas Ranger kati ya vipindi vingine na filamu.
Katika kumwomboleza mume wake, mkewe amemtaja marehemu kuwa mtu aliyejitolea kama mume wake mbali na kujitolea katika kazi zake za kucheza filamu akieleza kwamba upendo aliokuwa nao utakumbukwa daima.
“Art hakuwa tu muigizaji mzuri lakini pia alikuwa mume aliyejitolea, rafiki na chanzo cha mwanga kwa kila mtu aliyemjua. Kicheko chake, shauku na upendo wa maisha utakumbukwa sana. Ijapokuwa mioyo yetu ni mizito, tunasherehekea urithi wa furaha na msukumo anaotuachia.” Alisema mkewe Art, Babe Evans.
Manguli wengine katika tasnia ya filamu nchini Marekani waliofanya kazi na ‘Leslie Barnes’ ikiwemo waelekezi na waandishi wa filamu pia wamemwomboleza msanii huyo wa filamu.
Katika siku zake za mwisho, ‘Barnes’ alikuwa msanii wa sauti
katika kipindi cha vibonzo cha The Proud Family: Louder and Prouder
kinachozalishwa na Disney+.