
Rapa maarufu wa Marekani A$AP Rocky ameondolewa mashtaka mawili ya kutumia silaha kwa nia ya kushambulia katika kesi iliyomhusisha na tukio la ufyatuaji risasi mwaka wa 2021.
Baada ya uamuzi huo kutangazwa siku ya Jumanne, msanii huyo aliruka kwa furaha na kukimbilia mpenzi wake, Rihanna, ambaye alikuwepo mahakamani.
Jopo la majaji jijini Los Angeles lilimwachia huru Rocky, ambaye jina lake halisi ni Rakim Mayers, baada ya takriban saa tatu za mashauriano. Endapo angepatikana na hatia, rapa huyo alikabiliwa na kifungo cha hadi miaka 24 jela.
Mara tu uamuzi ulipotangazwa, Rocky alionyesha hisia kali za furaha, akitabasamu kwa upana kabla ya kumkumbatia Rihanna kwa nguvu.
Katika video zinasosambazwa mitandaoni, inaonekana kuwa nyota huyo wa muziki hakuweza kuficha furaha yake, huku Rihanna akionekana kububujikwa na machozi ya faraja.
Kesi hiyo ilitokana na madai kwamba Rocky alifyatua risasi wakati wa ugomvi na aliyekuwa rafiki yake, Terell "A$AP Relli" Ephron, mnamo 2021 katika eneo la Hollywood.
Hata hivyo, upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha madai hayo bila shaka yoyote, na hivyo mahakama ikamuachilia huru.
Kwa sasa, Rocky anaweza kuendelea na maisha yake bila hofu ya kifungo, huku mashabiki wake wakisherehekea uamuzi huo kama ushindi mkubwa kwake na familia yake.