logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ngumi ya Sugunyo yaongeza nuru kwenye nyota ya Mandonga, azawadiwa gari la pili

Bondia huyo ambaye alishindwa kuzuia furaha yake alitoa shukran za dhati kwa bosi wa kampuni hilo lililomtunuku gari.

image
na Radio Jambo

Habari21 January 2023 - 11:18

Muhtasari


•Mandonga aliongezewa gari lingine jipya aina ya Subaru kwenye gereji yake, siku chache tu baada ya kuzawadiwa gari lingine aina ya Toyota Nadia.

•Mandonga alisema kwamba gari la kwanza ataachia familia yake kutumia huku yeye akitumia Subaru kwa shughuli zake.

Bondia mcheshi kutoka Tanzania Karim Mandonga ni mmiliki wa magari mawili mapya ambayo alizawadiwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Mnamo Alhamisi, Mandonga aliongezewa gari lingine jipya aina ya Subaru Imprezza kwenye gereji yake, siku chache tu baada ya kuzawadiwa gari lingine aina ya Toyota Nadia na mfanyibiashara wa Tanzania, Dick Sound.

Huku akizugumza na wanahabari baada ya kukabidhiwa gari lake la pili, bondia huyo aliyejawa na mbwembwe nyingi alisema kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kilimo, Mo Green International Company alimpeleka kwenye chumba cha maonyesho ya magari na kumtaka achague gari analotaka.

"Namshukuru Mungu. Gari nililochagua mimi, nimechagua mnyama mmoja wa ajabu. Yaani ni Subaru matata, toleo jipya. Mandonga Mtu Kazi natembelea gari jipya la kitajiri na la kifahari," Mandonga alisema.

Bondia huyo ambaye alishindwa kuzuia furaha yake alitoa shukran za dhati kwa bosi wa kampuni hilo lililomtunuku gari.

"Wakati wa Mungu ndio wakati wa sahihi. @mogreeninternationalcompany boss sijui ata niseme kitu gani boss wangu ila Mungu atakulipa mara nyingi zaidi," aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mandonga alisema kwamba gari la kwanza ataachia familia yake kutumia huku yeye akitumia Subaru kwa shughuli zake.

Siku chache zilizopita Mandonga alimiliki gari kwa mara ya kwanza ambalo alizawadiwa kufuatia ushindi wake dhidi ya Mkenya Daniel Wanyonyi katika pambano lililochezwa katika ukumbi wa KICC Jumamosi iliyopita.

Bondia huyo mwenye maneno na tambo za mbwembwe alikabidhiwa zawadi aliporejea nchini Tanzania baada ya pambano lisilo la ubingwa dhidi ya Wanyonyi. Alishinda kwa TKO, ushindi ambao ulimpa heshima nyingi.

Namshukuru Mungu nilicheza kama niko Tanzania, nilitangaza ngumi yangu ya kigeni ikitoka Ukraine inaitwa Sugunyo, nashukuru mwenyezi mungu kwa hatua aliyonipa', alisema Mandonga baada ya kukabidhiwa gari hiyo.

Ushindi dhidi ya Daniel Wanyonyi ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa bondia huyo wa Bongo kucheza nje ya Tanzania.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved