Mjukuu wa Kibaki, Sean Andrew azungumza kuhusu kuingia kwenye siasa

Sean Andrew ameweka wazi wazo lake kuhusu kuwahi kujiunga na siasa katika siku za usoni.

Muhtasari

•Kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana kutupilia mbali uwezekano wa yeye kujiunga na ulingo huo mgumu.

•Sean ni mwanawe Jimmy Kibaki, mtoto wa pili wa hayati Kibaki. 

Sean Andr3w
Image: HISANI

Mtayarishaji wa Maudhui maarufu wa Kenya Sean Andrew, mjukuu wa hayati Emillio Mwai Kibaki ameweka wazi wazo lake kuhusu kuwahi kujiunga na siasa.

Wakati akiwashirikisha wafuasi wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumapili, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana kutupilia mbali uwezekano wa yeye kujiunga na ulingo huo mgumu.

Mtumiaji mmoja wa Instagram alimuuliza mjukuu huyo wa Kibaki ikiwa huwa anapata mawazo ya kujihusisha kikamilifu na siasa.

"Je, unawahi kufikiria kujihusisha na siasa au labda kujiunga na siasa?" shabiki aliuliza.

Sean alijibu swali hilo kwa video ikimuonyesha akitikisa kichwa upande kwa upande, ishara inayotumiwa kuashiria "Hapana."

Kuna uwezekano mkubwa kuwa shabiki huyo aliuliza swali hilo ili kujua ikiwa mtayarishaji wa maudhui huyo mrembo atawahi kupanga kufuata nyayo za babu yake ambaye alihudumu kama rais wa Kenya kwa mihula miwili kati ya mwaka wa 2002 na 2013.

Katika mahojiano ya takriban miaka miwili iliyopita, Be Andrew alibainisha kuwa hana mpango wa kujitosa kwenye ulingo wa siasa kama marehemu babu yake.

Alisema kuwa anaridhika zaidi kutoa mchango wake kwa Wakenya kama raia wa kawaida, jambo ambalo anakusudia kuendelea nalo.

"Sioni haja ya siasa katika maisha yangu. Nadhani naweza kuwasaidia Wakenya zaidi nikiwa kama raia wa kawaida. Mtu yeyote anaweza kuboresha maisha ya Wakenya, sio wanasiasa tu," Alisema.

Sean alihojiwa takriban miezi miwili baada ya kifo cha hayati Mwai Kibaki ambapo alisema bado hakuwa ameweza kukabiliana na majonzi.

Mwanamitindo huyo hata hivyo alipongeza upendo mkubwa ambao Wakenya walimuonyesha wakati alipompoteza babu yake.

"Sisi Wakenya tunashirikiana sana. Nilifurahia sana kupokea upendo mkubwa kutoka kwa Wakenya wakati wa kipindi kigumu ambacho tulipitia sote. Nina raha na tuendelee na tamaduni hiyo," Alisema.

Sean Andrew ni miongoni mwa watu maarufu zaidi kutoka familia ya aliyekuwa rais wa tatu wa Kenya. Yeye ni mwanawe Jimmy Kibaki, mtoto wa pili wa hayati Kibaki.