Mfanyabiashara maarufu Being Amira amewapuuza vijana ambao wamekuwa wakipiga kambi katika DM zake kwa nia ya kumtongoza.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Amira amedokeza kuwa kuna vijana wengi ambao wamekuwa wakijaribu bahati yao kwake baada ya kutengana na Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki Matatu jijini Nairobi Jimal Marlow Rohosafi
Hata hivyo amewataka vijana hao kukoma kumtumia jumbe huku akiwabainishia kuwa hana chochote cha kuwapatia.
"Wavulana hawa wote wadogo wanaonitumia meseji wakisema Hey na Hello. Sina biskuti za kuwapa," Amira alisema kwenye Instastori.
Haya yalijiri siku moja tu baada ya mfanyibiashara huyo kudokeza kuwa huenda hisia zake kwa Jimal tayari zimekwisha.
Kwenye Instagram, Amira alipakia picha yenye maandishi, "Utashtushwa na jinsi ambavyo mtu hukosa mvuto kwako mara somo linapopatikana."
Chini ya picha hiyo aliandika, "Mpenzi wake wa zamani huwa sio wa aina yake tena."
Wanamitandao wengi walitafsiri chapisho hilo kuwa ujumbe wa moja kwa moja kwa aliyekuwa mume wake Jimal Rohosafi.
Katikati ya mwezi uliopita, Jimal aliandika ujumbe mrefu wa kuomba msamaha kwa Amira na kukiri kuwa alimkosea sana mama huyo wa watoto wake wawili kwa kuingiza drama nyingi kwenye ndoa yao ya miaka mingi.
"Naomba radhi kwa kukukosea heshima, kukuaibisha, kwa kukuumiza, kwa maumivu yote na kwa huzuni niliyokuletea. 💔Samahani kwa nyakati zote ambazo sijawa mwanaume niliyeahidi kuwa," Jamal alimuandikia mkewe.
Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wamiliki Matatu jijini Nairob alikiri kwamba alikosa kutimiza wajibu wake wa kumlinda mkewe kama alivyohitajika kufanya.
Aidha alikiri kuwa alifahamu wakati ndoa yake ikiporomoka ila akashindwa na la kufanya kwa wakati ule.
"Ilikuwa mbaya kabisa. Huenda nilionekana kama mtu asiye na wasiwasi lakini sikuwa na la kufanya. Nilijua haikuwa sawa, nilijua unaumia lakini sikuweza kujikusanya!Amira nafanya hivi kwa sababu ukosefu wa heshima pia ulikuwa mkubwa. Naomba radhi kwa kukosa heshima," Aliandika.
Jimal pia alifichua kuwa hajakuwa sawa tangu alipokosana na mke huyo wake. Pia alidokeza kuwa yupo tayari kupiga hatua zozote ili kufufua ndoa yao iliyokufa miezi kadhaa iliyopita.
"Tafadhali nisamehe. Mimi na wewe tumetoka mbali na kukupitishia kwa yote hayo hakukuwa kuzuri. Tafadhali nisamehe Amira,"
Katika jibu lake, Amira alisema kwa wakati huo hangeweza kuuelewa msamaha wa mumewe kwani ulifufua kumbukumbu ya siku mbaya za nyuma.
"Ombi hilo la msamaha limenirudisha katika sehemu moja ya giza ambayo nimewahi kuwa katika maisha yangu kwa sababu nimetafakari juu ya mengi yaliyotokea hadharani na nyuma ya milango iliyofungwa na imezua hisia nyingi," Amira alijibu.
Mama huyo wa watoto wawili aliomba neema ya Mungu wakati akiendelea kutafakari suala hilo na kueleza kuwa kwa wakati huo alizidiwa na hisia.
"Vidonda vingine haviponi, lazima ujifunze jinsi ya kuishi navyo," Aliandika.
Mwaka jana ndoa ya Jimal iliingiwa na doa baada yake kujitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanasoshalaiti Amber Ray.
Jimal alimchukua Amber Ray kama mke wake wa pili, hatua ambayo ilisababisha drama zisizoisha kwenye ndoa yake.
Mfanyibiashara huyo alikumbwa na mkanganyiko kuhusu amchague nani wakati wake wake wawili walipoanza kuzozana..
Baadae aliamua kumchagua Amber Ray, jambo ambalo lilimkera Amira ambaye mwezi Novemba alianza mikakati ya talaka.