Staa wa Bongofleva, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameibua malalamiko yake baada ya wimbo wake mpya ‘Sherehe’ kushushwa kwenye mtandao wa YouTube.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alidai kuwa aliyesababisha kufutwa kwa wimbo wake ni msanii wa Kenya.
Alibainisha kuwa sio mara ya kwanza kwa wimbo wake kushushwa wakati ukivuma baada ya msanii wa Kenya kuwasilisha malalamiko yake kwenye YouTube.
“Hii sio mara ya kwanza!! Kushusha wimbo kipindi unaanza kuwa na moto unashushwa YouTube na mara kadhaa tukifuatilia unakuta mtu anajitambulisha anatoka Kenya,” Harmonize alilalamika.
Aliendelea, “Ninachojua ni kuwa Wakenya wanampenda na kumuunga mkono sana Konde Boy!! Day 1, siku zote tuko pamoja. Ombea Kenya. Kama unakumbuka vizuri wakati natoa #UNO 2020 ilishushwa na produsa ambaye inasemekana ni Mkenya. Aliweza kuuamini mtandao wa YouTube kuwa wimbo ni wake mpaka alipogundua sio sawa akaomba radhi hadharani!”
Msanii huyo wa zamani wa WCB alieleza kuwa wimbo huo ulishushwa wakati yeye na timu yake wakirekodi video yake.
“Pole kwa wanaKondegang wote, timu inajitahidi kulishughulikia suala hili kabla ya video kutoka!! Hakuna tunachoweza kumfanya, nina uhakika bado ni shabiki mkubwa, na hichi anachokifanya nakitafsiri kama upendo wa aina nyingine,” alisema.
Katika video ambayo alichapisha, Konde Boy alifichua kuwa aliamka saa kumi asubuhi ili kushoot video ya wimbo huo lakini akakuta umeshushwa.