Sekta ya elimu hapa nchini Kenya imekumbwa na hali ya sintofahamu baada ya zaidi ya vyuo vikuu vitano kuhusika na migomo kwa sababu tofauti.
Chuo Kikuu cha Kenyattta kilianzisha msafara huu huku kikifuatwa na chuo kikuu cha masinde Murilo. Chuo Kikuu cha Pwani pia kimejiongeza kwenye orodha hii. Hizi hapa ni sababu tano ambazo zimekuwa katika mstari wa mbele kusababisha janga hili;
- Ongezeko la Karo
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Kenyatta na pwani walizua malalamishi kuhusu ongezeko la karo. Vyuo vingi hapa nchini Kenya zimeongeza karo yake kutokana na hali ya kiuchumi inayoshuhudiwa humu nchini. Jambo hili limewapandisha mori wanafunzi, huku wengine wakiamua kueleza gadhabu zao kupitia njia za migomo.
- Ukosefu wa alama
Kila mwanafunzi katika chuo kikuu ana matumaini makubwa ya kuhitimu kwa muda na wakati unaofaa. Hata hivyo, wanafunzi wengi wamejikuta katika jinamizi la ukosefu wa alama na hivyo kupelekea wengi wao kukosa kuhitimu vyuo vikuu kwa wakati unaofaa. Jambo hili limechangiwa na mambo mengi huku wahadhiri wa vyuo hivi wakiwa chanzo kikuu chake. Pamoja na hayo, Idara za shule mbalimbali pia zimekua na matatizo mengi ambayo yamepelekea wanafunzi wengi kukosa alama. Jambo hili limekua chanzo cha matatizo mengi vyuoni hapa nchini Kenya.
https://radiojambo.co.ke/jumatatu-sio-sikukuu-puuzeni-taarifa-wizara-yasema/
- Ziara za kitaaluma
Chuo kikuu cha pwani kilijipata katika hali ya sintofahamu baada ya wanafunzi wa mwaka wa nne kudai hela zao za safari za kielimu. Kila chuo kikuu huwapeleka wanafunzi wake katika ziara za kitaaluma kabla hawajahitimu chuo. Hata hivyo, vyuo vingi hapa nchini vimekuwa vikiwadai wanafunzi hela za ziara hizi na baadae kuelekea kukamilisha chuo bila safari zenyewe kutimiza.
- Ufisadi
Ufisadi umekua janga kuu humu nchini. Jinamizi hili limeingia kwenye vyuo vikuu pia na mfano mzuri ni “The Mara Heist”. Vyuo vingi humu nchini vimewanyima wanafunzi wake ripoti kamili ya utumizi wa fedha humo ndani. Wanafunzi katika chuo kikuu cha Maasai Mara bado hawajepewa ripoti kamili kuhusu utumizi wa hela humo chuoni. Jambo hilo limesababisha hali ya mshikemshike hapa na pale baina ya shule na wanafunzi.
- Ukosefu wa rasilimali
Vyuo vingi humu nchini havina rasilimali za kutosha zitakazo wezesha kuendeleza baadhi ya kozi vyema. Chuo kikuu cha pwani kililalama kuhusu ukosefu wa viti ndani ya madarasa.
Wanafunzi wengi walilazimika kurejea nyumbani baada ya kukosa viti vya kukalia madarasani. Chuo kikuu cha Tum, Kenyatta pamoja na Masinde Murilo pia vimekua katika hali hii. Wanafunzi wake wamesikika wakilalama kuhusu ukosefu wa rasilimali za kutosha za kuendeleza elimu yao.
Habari na, Albanus Kiswili: Twitter: @Albanus_10