Mwiba kujidunga hauambiwi pole . sasa waliotoa msemo huo walijua wanachosema na ndio hali ambayo Maria Khatuve anajipata .
Alikosa msimamo wakati kaka wawili walipoanza kumtongoza na kwa sababu ya tamaa anasema alianza kuoyesha ishara za kuwakubali wote huku kila mmoja akizidi kumkaribia . sasa tatizo ni kwamba kaka hao hawajui kwamba Maria anazungumza na mwingine . Imefika wakati wote wawili wanataka kumuoa . Maria ameshindwa atafanya nini kwa sababu alifikiri mwanzoni kwamba ni utani lakini anapofuatilia mambo ,anagundua kwamba kaka hao wanataka kufanya harusi yao kwa pamoja ,siku moja na wameshaambiana kuhusu uhusiano wao na mwanamke wanayempenda bila kujua kwamba ni mwanamke mmoja .
Maria amekuwa na woga wa kuwaambia kaka hao kwamba alifanya kosa kwa kuedelea kuzungumza nao na kuwapa wote matumaini kwamba amewakubali katika uhusiano ambao sasa umepiga takriban miaka miwili . Aliwajua wakati mmoja na kila mmoja akachukua nambari yake ingawaje wakati tofauti na hapo ndipo ngoma hiyo ilipoanzia .
Maria anasema mwanzoni alifikiri kaka hao walikuwa wanajua wanachofanya kwani jumbe zao na hata mazungumzo kati yake nao yalikuwa yakifanyika wakati sawa na akajua wanamchezea shere lakini baadaye aligundua kwamba walikuwa wanaishi miji mbali mbali na hivyo basi hawakujua kwamba wanazungumza na mwanamke mmoja .
Amekutana nao kwa deti lakini kamwe hakuthibutu kujisema akihofia kwamba huenda angewatenganisha au kuwapoteza wote . lengo lake anasema lilikuwa kutumia muda mrefu kadri ya uwezo wake kumtambua aliye bora kati yao kisha kumueleza mwingine kuhusu kinachofanyika lakini amejipata kuwapenda wote kwa njia sawa kwani kila mmoja na sifa zake nzuri na udhaifu wake . Maria sasa amekanganywa na kaka hao wa familia moja lakini kwa sababu kila mmoja amepiga hatua ya kutaka kuwasilisha posa anajua wakati umewadia kwa kusema ukweli lakini bado anaogopa matokeo ya hatua yake ya kusema ukweli .
