JE, RAIS YU SALAMA?

Hawana bahati huko Lucky Summer!

Juhudi za kumsimamisha rais ziliangukia patupu kwani msafara uliendelea na safari bila ya rais kuwahutubia wenyeji kama walivyotarajia.

Muhtasari

•Msemaji wa serikali kupitia mtandao wa Twitter alitangaza kuwa mwanaume yule alikuwa tu amesisimka kuona msafara wa rais na akahakikishia Wakenya kuwa hakukuwa na tishio lolote kwa  usalama wa Rais.

Msafara wa Rais Kenyatta
Msafara wa Rais Kenyatta
Image: HISANI: YOUTUBE

Msafara wa Rais ulilazimika kusimama ghafla baaada ya mwanaume mmoja upande wa Lucky Summer kusimama mbele ya gari linaloaminika kumbeba rais siku ya Jumatano.

Kwenye video inayozunguka mitandaoni, kikundi cha watu waliokuwa wamesimama kando ya barabara kinaonekana kujaribu kutambua gari haswa iliyobeba rais kwenye msafara huo na wakati wanaridhika kuwa gari fulani ndiyo imembeba rais, mwanaume mmoja jasiri anajitolea kuenda mbele ya gari hilo ili kulisimamisha. Tazama video hapa chini

Magari hayo yanaonekana kupunguza mwendo kutokana na tukio hilo kisha maafisa ambao walikuwa wamemuandama rais wanamfurusha mwanaume huyo kutoka kwa barabara.

Kikundi kikubwa cha watu kilichokuwa kinajiangalilia msafara huo kiliskika kikishangilia mwanaume huyo kwa ujasiri wake huku wengine wakinyooshea magari hayo mikono ili yasimame.

Hata hivyo, juhudi hizo za kumsimamisha rais ziliangukia patupu kwani msafara huo uliendelea na safari punde baada ya mwanaume huyo kuondolewa barabarani na rais hakusimama kuwahutubia wenyeji wale kama walivyotarajia.

Baadae, msemaji wa serikali kupitia mtandao wa Twitter alitangaza kuwa mwanaume ule alikuwa tu amesisimka kuona msafara wa rais na akahakikishia Wakenya kuwa hakukuwa na tishio lolote la usalama wa Rais.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha wiki moja tukio kama hilo kutokea baada ya mwanaume mwingine kumkaribia rais Kenyatta akitoa hotuba yake na kwenye hafla ya kuzindua bandari ya Lamu. Rais alionekana kushtuka kidogo kutokana na tukio lililofanyika Alhamisi iliyopita.

Rais alikuwa anaelekea kuzindua kichinjio upande wa Neema, Nairobi.