UHURU DHIDI YA MAHAKAMA

Kuria, Karua wamkosoa rais kwa kutishia idara ya mahakama

Rais Kenyatta alisema kuwa idara ya mahakama imejaribu mipaka ya katiba ya Kenya kutoka kutupilia mbali matokeo ya kura ya urais 2017 hadi kutupilia mbali mchakato wa BBI

Muhtasari

•Kuria alisema kuwa hata Moi mwenyewe hakuwa na uhasama wowote na hakutishia idara ya mahakama

•Karua alisema kuwa kitendo cha rais kutishia idara ya mahakama ni cha aibu

Rai Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria na aliyekuwa mbunge wa Gichugu na mgombeaji wa kiti cha urais kwa wakati mmoja, Martha Karua wamekashifu Rais Uhuru Kenyatta vikali kwa kutishia idara ya mahakama.

Kupitia mitandao ya kijamii, Kuria amwambia Rais kuwa anafaidika kwa kutia machungu kwenye nchi.

"Hata Moi hakuwa na uhasama na hakutishia mahakama. Haswa kwenye siku ya Madaraka, Hapana. Wewe ndiye unayefaidika kwa kutia uchungu kwenye nchi, inashtua! inaogofya! Kaeni macho Wakenya" Kuria aliandika.

Kwa upande wake Karua, amesema kitendo cha rais Kenyatta kutishia idara ya mahakama ni aibu kubwa sana huku akisema kuwa Kenya ni ya kila mtu ila sio ya walio uongozini.

"Lazima Kenya iamke kutoka kwa vitisho ili kuwezesha haki kutendeka kwa waliopewa jukumu hilo na katiba. Rais Uhuru Kenyatta aweza kosa kupenda ukweli kuwa katiba inapunguza nguvu ya walio uongozini" Karua alichapisha kwenye mtandao wa Twitter.

Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha Madaraka Day ya 58 siku ya Jumanne mjini Kisumu, Rais Kenyatta alisema kuwa idara ya mahakama imejaribu mipaka ya katiba ya Kenya huku akiikashifu idara hiyo kwa kutupilia mbali mchakato wa BBI.