UVIVU NA UJEURI

Laikipia: Wauguzi 2 wapigwa kalamu baada ya mwanamke kufariki walipohudhuria sherehe

Mgonjwa alielezwa asubiri kwani wauguzi na wahudumu wa maabara walikuwa wameenda kuhudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa

Muhtasari

•Mwanamke, 58, aliaga alipokuwa anasubiri kuhudumiwa na wahudumu ambao walikuwa wameenda kuhudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya mhudumu mwenzao katika hospitali ya Nanyuki Teaching & Referral.

Mhudumu wa maabara akihojiwa kutokana na kifo cha mgonjwa
Mhudumu wa maabara akihojiwa kutokana na kifo cha mgonjwa
Image: Hisani

Wahudumu wa afya wawili wamekomeshwa kazi baada ya mwanamke mmoja kufariki alipokuwa anasubiri kuhudumiwa katika hospitali moja kaunti ya Laikipia.

Imeripotiwa kuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 58 aliaga alipokuwa anasubiri kuhudumiwa na wahudumu ambao walikuwa wameenda kuhudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya mhudumu mwenzao katika hospitali ya Nanyuki Teaching & Referral.

Mwanawe marehemu amesema kuwa ombi lake kwa wahudumu hao kuwataka wahudumie mama yake liliangukia patupu licha ya hali ya marehemu kuendelea kuzorota.

Alisema kuwa mamaye ambaye alihitaji kupewa damu alikuwa amepelekwa katika kitengo cha hali mahututi siku ya Jumatatu na kuandikiwa vipimo mbalimbali.

Hata hivyo, walielezwa wasubiri kwani wauguzi na wahudumu wa maabara walikuwa wameenda kuhudhuria sherehe.

Siku ya Ijumaa, wakuu wa afya katika kaunti ya Laikipia walisema kuwa walikuwa wamefanya uchunguzi na wakagundua kuwa marehemu alikuwa na matatizo mengi ila kulikuwa na uvivu na ujeuri miongoni mwa wahudumu wa maabara.

"Mabadiliko yamefanyika katika idara ya maabara na wawili wa wahudumu ambao walipatikana na hatia wamechujwa huku tukisubiri upelelezi zaidi" ujumbe kutoka kwa mtendaji katika wizara ya afya kaunti hiyo, Rose Maitai ulisoma.

(Tafsiri na Samuel Maina)