SOMALIA VS KDF

Somalia yalaani vikali matendo ya jeshi la KDF

Serikali ya shirikisho la Somalia imedai kuwa wanajeshi wa KDF wanafanya mashambulio ya angani kiholela yanayoangamiza na kuua raia wasio na hatia

Muhtasari

•Wametaja shambulio linalodaiwa kufanyika maeneo ya El-Adde na Hisa-u-gur yaliyo katika jimbo la Jubaland siku ya Alhamisi ambalo linasemekana kusababisha maafa na majeraha kwa raia haswa watoto na wanawake.

•Somalia imekuwa ikilalamikia matendo ya jeshi la KDF ya kuua raia na kuharibu mali mara kwa mara.

Ndege ya KDF
Ndege ya KDF
Image: Maktaba

Serikali ya Shirikisho ya Somalia imelaani vikali jeshi la Kenya almaarufu kama KDF kwa madai kuwa wanajeshi hao wanafanya mashambulio ya angani yanayoumiza na kuua raia wasio na hatia.

Serikali hiyo imeeleza kuwa operesheni zinazofanywa na jeshi la KDF zinafanyika kwa njia inayokosa kuwiana na wajibu waliopewa na shirika la umoja wa mataifa kupitia baraza la usalama.

Nchi ya Somalia imesema kuwa jeshi la KDF limekuwa likikiuka kipengele kinachoamuru wanajeshi wa AMISOM kutekeleza majukumu yao kisheria na kulinda raia haswa wanawake na watoto.

Wametaja shambulio linalodaiwa kufanyika maeneo ya El-Adde na Hisa-u-gur yaliyo katika jimbo la Jubaland siku ya Alhamisi ambalo linasemekana kusababisha maafa na majeraha kwa raia haswa watoto na wanawake.

"Inakuwa dhahiri kuwa mtindo wa uchochezi na kiholela ambao KDF inatumia kufanya operesheni zake Somalia wakidai kuwa wanapigana na misimamo mikali hautafanikisha kuleta utulivu na kukabiliana na misimamo mikali ila tu kubadilisha jamii zinazounga mkono misimamo mikali" Serikali ya Somali ilisema kupitia ujumbe wa kuchapishwa.Wamesema kuwa mali na raia hawafai kamwe kuwa lengo la matendo ya kijeshi.

Somalia imekuwa ikilalamikia matendo ya jeshi la KDF ya kuua raia na kuharibu mali mara kwa mara.