KAMPENI ZA KIAMBAA

"Kifo cha Jubilee kilikuwa Juja, mazishi ni Kiambaa" -Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameeleza imani yake kuwa chama cha UDA kitatwaa ushindi wa zaidi ya asilimia 70% kwenye uchaguzi mdogo eneo bunge la Kiambaa.

Muhtasari

•Hata hivyo, Kuria amepongeza maafisa wa polisi, serikali na chama cha Jubilee kwa kuzingatia heshima na imani kwenye kampeni za eneo hilo

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria akizungumzia wanahabari katika eneo bunge la Kiambaa siku ya Jumapili
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria akizungumzia wanahabari katika eneo bunge la Kiambaa siku ya Jumapili
Image: Facebook

Mbunge wa Gatundu ya Kusini Moses Kuria ameeleza imani yake kuwa chama cha UDA kitatwaa ushindi wa zaidi ya asilimia 70% kwenye uchaguzi mdogo eneo bunge la Kiambaa.

Akizungumza na wanabari katika soko la Rivarori ambako wandani wa naibu rais William Ruto walikuwa wameenda kupigia mgombeaji John Njuguna depe siku ya Jumapili , mbunge huyo wa pili amesema kuwa chama cha Jubilee kiko katika hali mahututi kutokana na matokeo hafifu ambayo kimekuwa kikipata kwenye chaguzi ndogo zilizopita.

Kufikia saai mi naona hapa chama cha UDA kitapita na asilimia zaidi ya 80%, ikienda chini sana 70%. Tungependa kuambia chama cha Jubilee pole sana, kifo ilikuwa Juja mazishi ni Kiambaa” Kuria alitangaza.

Kiongozi huyo wa chama cha People’s Empowerment Party amejitosa katika kumpigia mgombeaji wa chama cha UDA deni baada ya kuondoa mgombeaji wake, Raymond Kuria kwenye kinyang’anyiro hicho awali mwezi uliopita.

Kuria pia amepongeza maafisa wa polisi, serikali na chama cha Jubilee kwa kuzingatia heshima na imani kwenye kampeni za eneo hilo.

Kinyume na vurugu zilizoripotiwa kwenye kampeni katika maeneo bunge ya Bonchari na Juja, Kuria amekiri kuwa hakuna matatizo yaliyoibuka katika maeneo ya Kiambaa.

“Kufikia sasa hatuna malalamishi yoyote. Ningependa kushukuru serikali kwa kuwa hatujasumbuliwa . Tunatumai vile tulivyoanza ndivyo tutakavyomaliza. Pia tumeshuhudia uhusiano mwema na vyama pinzani. Ningependa kushukuru chama cha Jubilee kwa kukubali kuondoa msafara wao ili tulipoagiza. Ningependa tuendelee kuonyesha  heshima kwenye kampeni zetu” Kuria alisema.

Kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika tarehe 18 mwezi Mei katika maeneo bunge ya Bonchari na Juja, vyama vya PEP, ODM na UDA vilitangaza kunyanyaswa na maafisa wa polisi waliodaiwa kutumwa na 'watu wakuu serikalini'

Chama cha ODM kilikuwa kimelalamika kuwa wawakilishi wake katika eneo la Bonchari walikuwa wamenyanyaswa na kukamatwa kiholela.

Katika eneo la Juja, wandani wa Ruto walilalamika kuwa maafisa wa polisi walikuwa wanatumika kusababisha vurugu wakati shughuli ya kuhesabu kura ilikuwa inaendelea

Tangu salamu za 'hand shake' kati ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, Kuria pamoja na wanasiasa wengine wanaomuunga mkono naibu rais walianza kujitenga na chama cha Jubilee ambacho kiliwasaidia kuingia bungeni mwaka wa 2017.

Hali katika chama hicho imeendelea kuzorota huku baadhi ya wabunge wakijitenga na chama hicho kabisa na kujiunga na chama cha UDA ambacho kinahusishwa sana na Ruto.

Chama cha Jubilee kimekashifiwa na vyama vingine mara kwa mara kwa kudaiwa kutumia nguvu katika kampeni na kwenye chaguzi.