MIZANI YA HAKI

Mwanajeshi Mmarekani apigwa faini ya 70,000 kwa kumshambulia polisi Gigiri

Inadaiwa kuwa Stanley alimshika konstabo Kamau shingoni, akamtoa barakoa kisha akamgonga kwenye jicho lake la kushoto kabla ya konstabo Henry Kibet ambaye walikuwa zamu naye kuja kumsaidia.

Muhtasari

•Zarnoch Stanley alikubali shtaka alilokabiliwa nalo mbele ya hakimu mkuu  katika mahakama ya Kibera, Charles Mwaniki  na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja iwapo atakaidi faini aliyotozwa.

•Alipokuwa anahukumiwa, aliagiza mahakama kumuonea huruma huku akidai kuwa alikuwa anatumia dawa kwani alikuwa anaugua.

Zarnoch Stanley katika mahakama ya Kibera
Zarnoch Stanley katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanaume mmoja ambaye  alikuwa mwanajeshi wa anga Marekani amepigwa faini ya Sh70000 kwa kushambulia afisa wa polisi.

Zarnoch Stanley alikubali shtaka alilokabiliwa nalo mbele ya hakimu mkuu  katika mahakama ya Kibera, Charles Mwaniki  na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja iwapo atakaidi faini aliyotozwa.

Stanley alishtakiwa kumshambulia konstabo Kamau Muthoni katika kiingilio cha ofisi za shirika la uhamisho zilizo Gigiri na kumpiga mangumi kwenye uso na mkono kisha kumkanyanga mguu mnamo  tarehe 2 mwezi huu.

Alikuwa ameandamana na mwanamke Mwafrika anayeaminika kuwa mpenzi wake na ambaye alikuwa na miadi katika ofisi za shirika uhamiaji wakati tukio hilo lilitokea. 

Mmarekani huyo alizuiliwa kupita baada ya mwenzake  kuingia kulingana na sheria za shirika lile na akaagizwa kumsubiri nje ya lango.

Kufuatia hayo, mwanajeshi huyo mstaafu alianza kumtishia Kamau huku akimtupia maneno machafu.

Inadaiwa kuwa Stanley alimshika konstabo Kamau shingoni, akamtoa barakoa kisha akamgonga kwenye jicho lake la kushoto  kabla ya konstabo Henry Kibet ambaye walikuwa zamu naye kuja kumsaidia.

Alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi kufuatia kitendo hicho.

Alipokuwa anahukumiwa, aliagiza mahakama kumuonea huruma huku akidai kuwa alikuwa anatumia dawa kwani alikuwa anaugua.