MCHAKATO WA BBI

Reggae itarudi! Raila ahakikishia Wakenya akiwa Nyeri

Raila alisema kuwa BBI ilikuwa zao la mapendekezo ya marekebisho ambayo timu yake imekuwa ikitoa hapo awali kwa manufaa ya Wakenya.

Muhtasari

•Raila alisema kuwa kusimamishwa kwa mchakato wa BBI katika mahakama kuu ni kama kipindi cha mapumziko kwenye mechi ya kandanda.

•Alisema kuwa ombi la umoja ambalo alikuwa akipigia debe na rais Uhuru Kenyatta litaendelea huku akirejelea nyakati ambazo Kenya ilikuwa imeungana kupigana na mkoloni.t

Raila Odinga akihutubia waombolezaji Nyeri siku ya Ijumaa
Raila Odinga akihutubia waombolezaji Nyeri siku ya Ijumaa
Image: Hisani

Habari na Moses Odhiambo

Kinara wa ODM, Raila Odinga alitangaza imani yake kuwa mchakato wa BBI utarejea baada ya kukamilika kwa kesi iliyo mbele ya mahakama ya kukata rufaa.

Raila alisema kuwa kusimamishwa kwa mchakato wa BBI katika mahakama kuu ni kama kipindi cha mapumziko kwenye mechi ya kandanda.

Alikuwa akihutubia waombolezaji upande wa Nyeri kwenye ibada ya mazishi ya Esther Ngonyo ambaye ni mama wa aliyekuwa meya wa Thika, Mumbi Ngaru siku ya Ijumaa.

Raila alikuwa ameandamana na mbunge wa Kieni, Kanini Kega miongoni mwa viongozi wengine wa maeneo hayo na akawasihi wakazi kuzingatia umoja kama ilivyokuwa siku za ukoloni.

Alisema kuwa ombi la umoja ambalo alikuwa akipigia debe na rais Uhuru Kenyatta litaendelea huku akirejelea nyakati ambazo Kenya ilikuwa imeungana kupigana na mkoloni.

"BBI iko katika kipindi cha mapumziko kwa sababu ya mahakama lakini nawahakikishia kuwa hakuna anayeweza kusimamisha reggea" Raila alisema.

Mgombeaji huyo wa kiti cha urais mara tano bila mafanikio alisimulia jinsi alimpigia debe Kibaki mwaka wa 2002 akieleza kuwa hiyo ni ishara tosha kuwa hana chuki na jamii ya Wakikuyu.

Alisema kuwa taifa lilikuwa limeungana siku ambazo babake alipigania kuwachiliwa huru kwa hayati Jomo Kenyatta.

Kiongozi huyo aliyekuwa waziri mkuu alieleza hofu yake kuhusiana na mgawanyiko ambao umekuwepo huku akisema kuwa Kenya ingekuwa imesonga mbele sana ikiwa viongozi walikubali kufanya kazi pamoja bila kuangazia ukabila.

Alisema kuwa hiyo hali hiyo ndiyo iliyompelekea kusema 'Kibaki Tosha' akieleza kuwa alimuona Kibaki kama Mkenya ambaye alikuwa na uwezo wa kutawala.

"Kwani sikujua Kibaki ni mkikuyu wakati nilikuwa nasema Kibaki tosha? Kwa bahati mbaya alihusika kwenye ajali . Nililazimika kutembea kote nchini wakati hakuwepo.. ni mimi nilikuwa nikiongoza kampeni  na tulishinda" Raila alisema

Raila alisuta sana dhana za mrengo wa siasa wa 'Hustler' akisema kuwa hazikuwa bora kuendeleza nchi.

Alisema kuwa hakuna mpango bora zaidi kuendeleza nchi mbele kama ule wa Vision 2030 ambao waliunda na aliyekuwa rais wa tatu, Mwai Kibaki.

Raila alisema kuwa BBI ilikuwa zao  la mapendekezo ya marekebisho ambayo timu yake imekuwa ikitoa hapo awali kwa manufaa ya Wakenya.