SUALA NYETI

22% ya vijana wa kati ya umri wa miaka 13-20 Kiambu wamewahi kushiriki ngono- Utafiti

Utafiti huo ulibaini kuwa 57% ya wasichana wenye umri wa ujana hushiriki tendo la ndoa kwa mara ya kwanza kutokana na udadisi.

Muhtasari

•Utafiti huo uliashiria kuwa 55.7% ya wasichana walizidiwa na hisia  ilihali 18.5% kati yao walibakwa.

•Utafiti huo uliashiria kuwa 81.9 ya vijana walioshiriki ngono walitamani kuzuia ujauzito ilhali 77.8% walitumia dawa za kuzuia ujauzito.

Mratibu wa masuala ya afya kaunti ya Kiambu, Davis Kamondo na mtafiti mkuu Profesa Peter Gichangi wakiwa Juja siku ya Jumatatu.
Mratibu wa masuala ya afya kaunti ya Kiambu, Davis Kamondo na mtafiti mkuu Profesa Peter Gichangi wakiwa Juja siku ya Jumatatu.
Image: JOHN KAMAU

Utafiti umebaini kuwa asilimia 22 ya vijana wa umri wa kati ya miaka 13 na 20 katika kaunti ya Kiambu wamewahi kushiriki ngono.

Utafiti huo ambao ulitekelezwa na shirika la Performance Monitoring for Action kupitia shirika la afya ya uzazi duniani ulifanywa kati ya mwezi wa Novemba na Desemba 2020.

Ulibaini kuwa 57% ya wasichana wenye umri wa ujana hushiriki tendo la ndoa kwa mara ya kwanza  kutokana na udadisi.

Asilimia 12.6 ya wasichana hao walisema kuwa walishiriki ngono kwani walihisi kwamba wanafanya walichotarajiwa kufanya ilhali 6% yao walisema kuwa walikuwa wamelewa wakishiriki mara ya kwanza.

Utafiti huo uliashiria kuwa 55.7% ya wasichana walizidiwa na hisia  ilihali 18.5% kati yao walibakwa.

Siku ya Jumatatu, mtafiti mkuu Peter Gichangi alisema kuwa suala la vijana kushiriki katika matendo ya ndoa ni suala nyeti na linafaa kushughulikiwa na sekta mbalimbali.

Alizungumza alipokuwa anawachilia matokeo ya utafiti wa utumizi wa mbinu za kuzuia uzazi za kisasa eneo la Kiambu.

Utafiti huo uliashiria kuwa 81.9 ya vijana walioshiriki ngono walitamani kuzuia ujauzito ilhali 77.8% walitumia dawa za kuzuia ujauzito.

Asilimia 9 ya wasichana wenye umri wa ujana wamewahi kujifungua ilhali asilimia 3 walikuwa wameolewa ama wanaishi na mwanaume kama kwamba wameoana, utafiti ulionyesha. 

(Utafsiri na Samuel Maina)