KILIO CHA HAKI

Hofu baada ya mwanafunzi wa KMTC kupatikana ameuliwa kinyama hostelini Homa Bay

Polisi wanamuwinda mpenzi wa marehemu ambaye kwa sasa hapatikani na amezima simu yake.

Muhtasari

•Mwili wa Emily Chepkemoi, 23, ulipatikana juu ya kitanda kilichokuwa ndani ya hosteli yake  huku umezingirwa na dimbwi la damu.

•Inatuhumiwa kuwa mpenziwe Chepkemoi ndiye alitekeleza unyama huo usiku wa Ijumaa.

Wanafunzi wa KMTC Homa Bay wamuomboleza mmoja wao aliyepatikana ameuliwa Jumapili
Wanafunzi wa KMTC Homa Bay wamuomboleza mmoja wao aliyepatikana ameuliwa Jumapili
Image: ROBERT OMOLLO

Hali ya mshtuko  na hofu imetanda katika chuo cha kufundisha masomo ya udaktari mjini Homabay (KMTC-Homabay Town)  baada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kupatikana ameuliwa siku ya Jumapili.

Mwili wa Emily Chepkemoi, 23, ulipatikana juu ya kitanda kilichokuwa ndani ya hosteli yake  huku umezingirwa na dimbwi la damu.

Majirani ambao walinusa harufu kali kutoka ndani ya chumba hicho waliamua kuvunja mlango na ndipo wakakumbana na mwili wa Emily ambaye alikuwa ameuliwa kinyama kisha wakaarifu maafisa wa polisi. 

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Homa Bay Teaching and Referral huku upasuaji wa mwili ukisubiriwa.

Ingawa haijabainika wazi aliyetelekeza kitendo hicho na kwa nini, polisi wanamuwinda mpenzi wa marehemu ambaye kwa sasa hapatikani na amezima simu yake.

Chifu msaidizi wa  mji wa Homabay, Duncan Okech alisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amedungwa kwa kisu mara mbili kwenye kichwa na shingo.

Inatuhumiwa kuwa mpenziwe Chepkemoi ndiye alitekeleza unyama huo usiku wa Ijumaa.

Kiongozi wa muungano wa wanafunzi katika chuo hicho, David Odhiambo aliagiza haki kutendeka na akaomba uchunguzi kamilifu kufanyika.

"Wanafunzi wengi walipatwa na mshangao na hawakuhudhuria madarasa yao kufuatia tukio hilo. Tunamuomboleza mmoja wetu na tunataka haki itendeke" Odhiambo alisema Jumatatu.

Maafisa wa DCI  walisema kuwa wanafuata miongozo muhimu ambayo wana matumaini itawaongoza waweze kutia mbaroni washukiwa wa mauaji hayo.