MAUAJI KAKAMEGA

MMUST: Hofu baada ya mwanafunzi kuuawa kinyama

Mwili wa Macrine Achieng, mwanafunzi wa shahada ya elimu, ulipatikana asubuhi ya kuamkia Jumatano ukiwa nusu uchi na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili.

Muhtasari

•Achieng alikuwa  katika mwake wake wa tatu akisomea shahada ya elimu,

•Mwili wa marehemu ulipatikana na alama kubwa kwenye kisogo, ishara ya kugongwa na kifaa butu na alama zingine kwenye mapaja.

Macrine Achieng
Macrine Achieng
Image: Hisani

Hali ya huzuni na hofu imetanda katika chuo kikuu cha Masinde Muliro(MMUST) baada ya mwanafunzi mmoja mwanamke kupatikana akiwa ameuliwa kinyama na kutupwa kichakani.

Mwili wa Macrine Achieng ambaye hadi mauti yake alikuwa mwanafunzi wa shahada ya elimu ulipatikana asubuhi ya kuamkia Jumatano ukiwa nusu uchi na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili.

Maafisa wa polisi wameanza upelelezi wao kubaini yaliyotokea huku ikituhumiwa kuwa huenda mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu alibakwa kabla ya kuuliwa kwani sehemu zake za siri zilikuwa na matone ya damu.

Wataalam wa kuchunguza mauaji wanafanya uchunguzi wao kubaini nini haswa kilisababisha mauti hayo huku ikituhumiwa huenda alipoteza damu nyingi mno baada ya kugongwa na kifaa butu kwenye kisogo.

Mwili wa marehemu ulipatikana na alama kubwa kwenye kisogo, ishara ya kugongwa na kifaa butu na alama zingine kwenye mapaja.

Imeripotiwa kuwa huenda marehemu aliuliwa ndani ya nyumba yake ya kukodishwa iliyo katika eneo la Kenfinco, viungani mwa mji wa Kakamega kabla ya mwili kubebwa na kutupwa mita kadhaa kutoka nyumba hiyo. Athari za damu zilionekana kutoka kwa nyumba kuelekea kwa ngazi za ploti hiyo.

Kulingana na mmoja wa waliofika kwenye eneo la tukio, mlango wa kuingia kwa nyumba ya Achieng haukuwa umefungwa wala kuwa na ishara zozote za kuvunjwa.

"Ni kama walikuwa na aliyemtendea unyama huyo kwa nyumba ama alidanganywa kufungua mlango kwani hakukuwa na ishara yoyote ya kuvunjwa kwa mlango huo na pia haikuonekana kana kwamba kuna chochote kilichokuwa kimeibiwa. Hata hivyo tuliweza kuona matone ya damu ndani ya nyumba hiyo" Ronnie ambaye ni mwanafunzi katika chuo hicho alieleza Radio Jambo.

Wanafunzi waliojawa na ghadhabu kutokana na mauaji ya mmoja wao waliandamana mitaani wakilalamikia ukosefu wa usalama.Hata hivyo, baada ya muda mfupi maafisa wa polisi waliwatawanya na kutuliza hali hiyo.

Anderson Kalu, mwanafunzi katika chuo hicho aliarifu radio jambo kuwa hicho sio kisa cha kwanza kuripotiwa katika maeneo ya Kefinco na Juakali. Angalau wanafunzi wawili wameuliwa maeneo hayo mwakani.

Mkutano wa seneti uliofanyika siku ya Jumatano ulipendekeza hatua kadhaa za kulinda usalama wa wanafunzi zikiwemo kuwekwa kwa mataa katika maeneo yaliyoathirika, kujengwa kwa kituo cha polisi katika maeneo ya Kefinco na Juakali, kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa wanafunzi na mengineo.

Muungano wa wanafunzi wa chuo hicho, MMUSO, umeagiza wanafunzi wanaoishi pande za Kefinco kuhama na kuwasihi kutembea kwa makundi haswa masaa ya usiku.