Mike Sonko ajitolea kuchukua na kulea watoto wa afisa Caroline Kangogo anayedaiwa kujitoa uhai

Bi Caroline Kangogo anadaiwa kuwa na watoto wawili wenye umri wa miaka 8 na 11.

Muhtasari

• Kwenye ujumbe ambao inatuhumiwa aliacha kama ameandika kabla ya kujitoa uhai, marehemu aliwaomba wazazi wake kuchukua majukumu ya wanawe wawili.

•Sonko alisema kuwa huenda kulikuwa na  matatizo kwenye uhusiano wake na wanaume wawili ambao alipiga risasi.

Image: HISANI

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi amejitolea kuwalea na kusomesha watoto wa afisa Caroline Kangogo anayedaiwa kujitoa uhai siku ya Ijumaa.

Sonko ametoa ombi kwa familia ya marehemu kuwa iwapo hawataweza kuwalea watoto wa Kangogo wamkabidhi majukumu yale kwani ako tayari kuwaajibikia.

Bi Caroline Kangogo anadaiwa kuwa na watoto wawili wenye umri wa miaka 8 na 11. Kwenye ujumbe ambao inatuhumiwa aliacha kama ameandika kabla ya kujitoa uhai, marehemu aliwaomba wazazi wake kuchukua majukumu ya wanawe wawili.

Kupitia mtandao wa Facebook, Sonko amesema kuwa watoto ni baraka kutoka kwa Mungu na hawafai kutelekezwa licha ya yaliyotendeka.

"Ombi langu kwa familia iliyo Elgeyo Marakwet, kama mutalemewa kusomesha au kulea watoto wake(Caroline) tafadhali nipatieni nikae nao nitawasomesha na kuwalea. Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu" Sonko aliandika.

Hapo awali Sonko alikuwa ameomba Wakenya kutohukumu Bi Caroline kama  mhalifu kwa kuua wanaume wawili akidai kuwa kwa wakati mwingine wanaume huwashinikiza wanawake kutenda maovu kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na matatizo kwenye uhusiano.

Alisema kuwa huenda kulikuwa na  matatizo kwenye uhusiano wake na wanaume wawili ambao alipiga risasi.

Mwanasiasa huyo alidai kuwa ingawa haungi mkono kujitoa uhai kwa Caroline, raia wangemkata wangemchoma hata bila kumpa nafasi ya kuongea yaliyo moyoni mwake.

"Haki gani ingine angepata? Kama raia wangemkamata wangemchoma hata bila kusikiliza ana yepi ya kusema kwani kesi yake ilichunguzwa na akashtakiwa kupitia mahakama ya maoni ya umma. Kwa kuwa sasa hayuko hai tena kila mtu anamhurumia!" Alisema Sonko.

Alisema kuwa marehemu alikuwa na haki ya kusikiwa kwanza kabla ya kuhukumiwa.