Mbunge Didmus Barasa akamatwa kwa madai ya kushambulia mwanakandarasi

Polisi walisema kuwa walikuwa wamepokea fomu ya P3 kutoka kwa mwanakandarasi huyo kufuatia tukio lililoibuka katika shule ya msingi ya Lurale Baptist

Muhtasari

•Barasa alikamatwa na maafisa wa polisi mapema asubuhi ya Jumatatu akiwa nyumbani kwake baada ya Masinde kumshtaki kwa kosa la shambulio

•Barasa anatuhumiwa kumshambulia Masinde na kumzaba kofi siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada yake kujaribu kumzuia kuzindua madarasa aliyokuwa amekarabati akidai hajapokea malipo.

Mbunge wa Kimilili Didimus Barasa
Mbunge wa Kimilili Didimus Barasa

Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amekamatwa kwa madai ya kumshambulia mwanakandarasi Stephen Masinde siku ya Ijumaa.

Barasa alikamatwa na maafisa wa polisi mapema asubuhi ya Jumatatu akiwa nyumbani kwake baada ya Masinde kumshtaki kwa kosa la shambulio.

Mbunge huyo anatarajiwa kusomewa mashtaka dhidi yake ya kusababisha majeraha mwilini wa Masinde ambaye pia ni mwanamuziki mashuhuri eneo la Magharibi mwa Kenya.

Polisi walisema kuwa walikuwa wamepokea fomu ya P3 kutoka kwa mwanakandarasi huyo kufuatia tukio lililoibuka katika shule ya msingi ya Lurale Baptist.

Fomu ya P3
Fomu ya P3
Image: JOHN NALIANYA

Barasa anatuhumiwa kumshambulia Masinde na kumzaba kofi siku ya Ijumaa wiki iliyopita baada yake kujaribu kumzuia kuzindua madarasa aliyokuwa amekarabati akidai hajapokea malipo.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto alipigwa na butwaa wakati alienda kuzindua madarasa hayo na kupata kuwa yalikuwa yamefungwa kwa kifuliali na hapo ndipo ghadhabu ikamshinikiza kumshambulia mwanakandarasi Stephen Masinde. 

Masinde almaarufu kama Steve Kay pamoja na mwanakandarasi mwenzake Ronald Graham walikuwa wameyafunga madarasa matano waliyokarabati katika shule ya msingi ya Lurare Baptist iliyo katika eneo bunge la Kimilili wakilalamikia kutolipwa shilingi milioni 3.4.

Wanakandarasi hao walisema kuwa juhudi zao za kumshinikiza Barasa kulipa hazikuwa zimefua dafu kwani mbunge huyo alikuwa akiwakwepa.

Masaa machache baadae Barasa alihudhuria mkutano mwingine katika shule ya msingi ya Namasanda na alipokuwa anahutubia waliohudhuria akachukua nafasi ile kutoa simulizi yake kuhusiana na yaliyojiri na kukanusha madai ya kumzaba kofi Masinde.

Barasa alisema kuwa mkanganyiko uliibuka wakati alienda kumuarifu Masinde afunge zipu ya suruali yake kwani kulingana na yeye ilikuwa wazi.

Alisema kuwa alipokuwa anaenda kwambia mwanamuziki huyo afunge zipu punde alipomuona alianza kutoroka akidhani kuwa alitaka kumpiga.

"..Kijana mwenyewe akakuja. Alafu kwa vile yeye ni rafiki yangu nikaona sijui alienda kujisaidia na alikuwa hajafunga zipu. Mimi naona gari yake ndogo iko ndani hajafunga nikasema wacha nikimbie nimwambie gereji yako iko wazi funga zipu! Funga duka! Sasa wakati nilifika pale kumwambia namna hivi akatoroka mbio akadhani nataka kumpiga" Barasa alisema.

Alisema kuwa mwanamuziki huyo alishindwa kutegua ishara alizojaribu kumwonyesha kuwa zipu yake ilikuwa wazi.

Barasa pia alikashifu kitendo cha mwanakandarasi huyo kufunga madarasa hayo akidai kuwa wanafunzi walilazimika kukaa nje baada ya Masinde kuwatoa ndani ya madarasa na kuyafunga.

"Hivo sivyo serikali inavyofanya kazi. Kama umefanya kazi na serikali  kuna utaratibu wa kufuatwa ili kupata pesa yako sio matendo kama yale yaliyopitwa na wakati" Barasa alisema.