Miujiza! Polisi aliyekuwa katika koma kwa miezi tisa aamka na kuzungumza

Alikuwa amevunjika mguu na jeraha kubwa kichwani.

Muhtasari

•Kwa kipindi cha miezi tisa Kimutai alikuwa amepoteza fahamu na hakusema neno lolote huku familia yake ikiendelea kumtafuta bila kujua alikuwa amelazwa hospitalini.

•Polisi ambao walikuwa wamempeleka hospitali hawakuwahi rudi kumwangalia tena na baadae akatangazwa kama afisa aliyekuwa ameacha kazi na mshahara wake ukaacha kulipwa.

•Alikuwa ameandikishwa kama ' mwanaume asiyejulikana' hadi tarehe 15 Septemba ambapo alizugumza na kudai kwamba yeye ni polisi.

Hospitali ya KNH
Hospitali ya KNH
Image: EZEKIEL AMINGA

Konstabo Reuben Kimutai Lel alikuwa anavuka barabara ya Jogoo jijini Nairobi mnamo Desemba 20, 2020 alipogongwa na gari na kuachwa katika hali mahututi.

Kimutai 59, ambaye alikuwa anafanya kazi katika mahakama ya Makadara alichukuliwa  na polisi kutoka eneo la tukio masaa kadhaa baadae na kupelekwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ambako aliandikishwa kama 'mwanaume asiyejulikana'

Alikuwa amepoteza fahamu na hakuwa na vitambulisho vyovyote mifukoni.

Madaktari katika hospitali ya KNH walimhudumia wakitumai kuokoa maisha yake. Alikuwa amevunjika mguu na jeraha kubwa kichwani.

Kwa kipindi cha miezi tisa Kimutai alikuwa amepoteza fahamu na hakusema neno lolote huku familia yake ikiendelea kumtafuta bila kujua alikuwa amelazwa hospitalini.

Hakuna aliyefahamu mahali alikuwa na kesi ya kupotea kwake ikaripotiwa katika kituo cha polisi cha Jogoo mnamo Januari 19.

Polisi ambao walikuwa wamempeleka hospitali hawakuwahi rudi kumwangalia tena. Baadae alitangazwa kuwa afisa aliyekuwa ameacha kazi na mshahara wake ukaacha kulipwa.

Kimutai alishtakiwa kortini kwa kuacha kazi kwa zaidi ya siku 10, kinyume na sheria.

Kesi hiyo ilikuwa kortini kwa miezi mitano lakini ikaondolewa baada ya polisi wenzake kushindwa kumpata.

Wasimamizi wa KNH walichukua alama zake za vidole na kubaini kwamba alikuwa ametoka eneo la Timboroa kaunti ya Baringo ili hawangeweza kumtambua virahisi kwani maelezo hayo hayakutosha.

Alikuwa ameandikishwa kama ' mwanaume asiyejulikana' hadi tarehe 15 Septemba ambapo alizugumza na kudai kwamba yeye ni polisi.

Familia yake ilisita kuzungumzia hayo na kusema kwamba wanafurahia kuona kwamba yuko hai.

Kimutai alikuwa amepelekwa kwenye wadi ya wagonjwa wa migupa ambapo alizungumza na kushangaza wengi.

Alisema kwamba yeye ni afisa wa polisi ambaye alikuwa anafanya kazi katika mahakama iliyo kwenye barabara ya Jogoo.

Wasimamizi wa hospitali walitumia maelezo hayo kufuatilia na wakaweza kuthibitisha madai yake.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema kuwa hafahamu kesi hiyo vizuri na akaomba apewe wakati wa kupata taarifa zaidi.

(Utafsiri: Samuel Maina)