Daktari anayedaiwa kuua wanawe wawili kwa kuwadunga sindano yenye sumu afariki akipokea matibabu Nakuru

Muhtasari

•James Muriithi Gakara ambaye alikuwa daktari wa uzazi katika hospitali ya Optimum Current Nakuru alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika chumba chake cha malazi siku ya Jumapili

Daktari James Muriithi Gakara anayeripotiwa kuua wanawe wawili
Daktari James Muriithi Gakara anayeripotiwa kuua wanawe wawili
Image: HISANI

Daktari kutoka Nakuru ambaye anatuhumiwa kuwaua watoto wake wawili amefariki alipokuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Nakuru Level 5.

James Muriithi Gakara ambaye alikuwa daktari wa uzazi katika hospitali ya Optimum Current Nakuru alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika chumba chake cha malazi siku ya Jumapili baada ya kujaribu kujitoa uhai.

Miili ya watoto wake wawili, mvulana wa miaka 5 na msichana wa miaka 3 ilikuwa imelala kitandani  huku povu ikichemka midomoni.

Inaaminika kuwa marehemu alikuwa amewadunga wanawe kwa sindano yenye sumu kabla ya kujaribu kujitoa uhai pia.

Dawa za aina tofauti , sirinji zilizokuwa zimetumika na kisu chenye makali ni baadhi ya vitu ambazo zilipatikana kwenye eneo la tukio.

Polisi walisema kuwa watoto wale walikuwa wamedungwa dawa ya insulini na huenda dawa zingine pia zilitumika kuwaangamiza.

Ilisemekana kuwa daktari huyo alikuwa amezozana na mkewe usiku wa Jumamosi.