Polisi ambaye alikuwa katika koma kwa kipindi cha miezi tisa apewa ruhusa kutoka hospitalini

Muhtasari

•Kimutai ambaye alikuwa anafanya kazi katika mahakama ya Makadara    alikuwa anavuka barabara ya Jogoo jijini Nairobi mnamo Desemba 20, 2020 alipogongwa na gari na kuachwa katika hali mahututi.

•Aliruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali ya Kenyatta siku ya Ijumaa na kupelekwa nyumbani kwake maeneo ya Koibatek kaunti ya Baringo ambako atakuwa anahudumiwa na familia yake.

•Baada ya kukosekana kazini kwa siku kadhaa,Kimutai alishtakiwa kwa kosa la kuacha kazi na baadae akapigwa kalamu

Konstabo Reuben Lel katika hospitali ya KNH kabla ya kupewa ruhusa
Konstabo Reuben Lel katika hospitali ya KNH kabla ya kupewa ruhusa
Image: FAMILIA

Afisa wa polisi ambaye aliamka baada ya kuwa amepoteza fahamu kwa kipindi cha miezi tisa amepewa ruhusa kutoka hospitalini.

Konstabo Reuben Kimutai Lel, 59,  aliruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali ya Kenyatta siku ya Ijumaa na kupelekwa nyumbani kwake maeneo ya Koibatek kaunti ya Baringo ambako atakuwa anahudumiwa na familia yake.

Mpwa wake Joan Jeptoo alisema kwamba hali ya Kimutai ya afya inaendelea kuimarika.

"Tutamchunga sasa na mengine yatafuata baadae" Jeptoo alisema.

Kimutai ambaye alikuwa anafanya kazi katika mahakama ya Makadara    alikuwa anavuka barabara ya Jogoo jijini Nairobi mnamo Desemba 20, 2020 alipogongwa na gari na kuachwa katika hali mahututi.

Alichukuliwa  na polisi kutoka eneo la tukio masaa kadhaa baadae na kupelekwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ambako aliandikishwa kama 'mwanaume asiyejulikana'. Hakuwa na vitambulisho.

Baada ya kukosekana kazini kwa siku kadhaa,Kimutai alishtakiwa kwa kosa la kuacha kazi na baadae akapigwa kalamu. Kesi hiyo imeweka walio mamlakani katika idara ya polisi taabani.

Hii ni kwa sababu maafisa wa polisi ndio waliita gari la kubebea wagonjwa kuchukua Kimutai na kumpeleka hospitalini ila baadae hawakufuatilia.

Suala hilo limekuwa likiangaziwa sana na polisi wengi  ambao wanahisi kwamba haikushughulikiwa jinsi ifaavyo.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema kwamba suala hilo linaashiria kuwa mabadiliko yanafaa kuwepo kuhusu namna suala kama hilo linafaa kushughulikiwa.

Shioso alisema kwamba suala la Kimutai kufutwa kazi na bili za hospitali zitashughulikiwa.

Kimutai alipata fahamu mnamo Septemba 15 ambapo aliamka na kuzungumza. 

Aliarifu madaktari kwamba yeye ni afisa wa polisi ambaye alikuwa anafanya kazi katika mahakama iliyo kwenye barabara ya Jogoo. Wasimamizi wa hospitali walitumia maelezo hayo kufuatilia na wakaweza kuthibitisha madai yake.

Familia na wafanyikazi wenzake walikuwa wakimtafuta bila mafanikio.

Kuna wakati ambapo familia yake ilichukua mwili uliokuwa unaoza ila  ishara za vidole hazikuwiana na za Kimutai. Familia yake ilipoteza matumaini ya kuwahi kumpata.

{Utafsiri: Samuel Maina}