Florence Muturi atajwa afisa mkuu mtendaji mpya wa LSK

Muhtasari

•Florence Wairimu Muturi ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji  mpya wa Chama cha Wanasheria wa Kenya.

•Yeye ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya mwenye tajriba ya zaidi ya miaka kumi na mitano


Florence Wairimu Muturi ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji  mpya wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, akichukua nafasi ya Mercy Wambua.

Wambua aliondoka madarakani Januari 2022 pamoja na aliyekuwa rais wa LSK Nelson Havi.

Wairimu alichaguliwa kutoka kwa orodha ya watu kumi katika kile ambacho chama hicho kinasema ni kupitia mchakato wa uwazi na wa ushindani.

Atahudumu kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2022.

Rais wa LSK Eric Theuri alisema kuwa Florence Muturi anawezaongezwa  muda tena wa kuudumu mara nyingine  baada ya  kudhibitisha utendakazi wake.

"Analeta maarifa na uzoefu katika uongozi na usimamizi," Theuri alisema.

 

Kabla ya uteuzi wake, Wairimu alikuwa kaimu Katibu/Mtendaji Mkuu wa LSK tangu kuteuliwa kwake Januari 2022.

Yeye ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya mwenye tajriba ya zaidi ya miaka kumi na mitano, baada ya kukula kiapo ya sheria mnamo tarehe 20 Julai, 2006.

Wairimu ana Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Moi, ana Diploma ya Usimamizi ya wafanyikazi na Katibu wa Umma aliyeidhinishwa.

Amehudumu katika Chama cha Wanasheria cha Kenya tangu 2012 kama Afisa Programu anayesimamia Idara ya Uzingatiaji na Maadili na baadaye kama Naibu Katibu/Mkurugenzi Mtendaji, kuanzia 2016.

“Baraza la Chama cha Wanasheria nchini Kenya linampongeza Bi Muturi kwa kuteuliwa na kumtakia kila la heri katika jukumu lake jipya,” Theuri alisema.