"Kumpoteza rais aliyekuwa madarakani kilikuwa kipindi kigumu’'-Mkuu wa Majeshi Tanzania

Muhtasari

•Mabeyo alieleza hayo katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV nchini humo.

.Rais Magufuli alifariki Machi 17, 2022, kutokana na matatizo ya moyo jijini Dar es Salaam.

Image: TWITTER

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (JWTZ) anayemaliza muda wake Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ametaja kifo cha Rais wa awamu ya tano John Magufuli kama moja kati ya changamoto kubwa alizokabiliana nazo katika kipindi cha utumishi wake.

Mabeyo alieleza hayo katika kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV nchini humo.

Alieleza kuwa hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kumpoteza rais aliyekuwa madarakani hivyo kilikuwa ni kipindi kigumu lakini kama Jeshi walisimama kidete kutimiza wajibu kwa mujibu wa katiba wa kuilinda nchi na katiba.

"Naamini kwamba tunaendelea vizuri, nchi iko salama mpaka sasa. Wananchi wako watulivu, wanaendelea kufuata miongozo kama inavyotolewa na Serikali,” aliongeza Mabeyo.

Rais Magufuli alifariki Machi 17, 2022, kutokana na matatizo ya moyo jijini Dar es Salaam.

Makamu wake wa rais wakati huo, Samia Suluhu Hassan, akarithi kiti chake kwa kuapishwa siku mbili tu baadaye , Machi 19, 2021 na kuwa Rais wa awamu ya sita na wa kwanza mwanamke katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Tanzania Venance Salvatory Mabeyo anatarajia kustaafu wadhifa wake mwisho mwa mwezi Juni, 2022, aliteuliwa kushika nafasi hiyo Februari 2017 na aliyekuwa rais wa awamu ya tano Hayati Dkt John Magufuli