Mauaji, mwanamume 27 amuua dadake mtaani Makongeni, Nairobi

Muhtasari

•  Alikamatwa saa chache baadaye na silaha ya muuaji ikapatikana. Polisi wanasema bado hawajabaini nia ya tukio hilo na wameanzisha uchunguzi tukio hilo.

Crime scene
Crime scene

Mwanamume mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa Alhamisi  jioni baada ya kumdunga kisu na kumuua dadake katika mzozo wa kinyumbani mtaani Makongeni, Nairobi.

Mshukiwa aliyetambulika kwa jina Patrick Mutunga alitumia kisu cha jikoni kumuua Sylvia Kamene baada ya ugomvi ndani ya nyumba yao.

 Alikamatwa saa chache baadaye na silaha ya muuaji ikapatikana. Polisi wanasema bado hawajabaini nia ya tukio hilo na wameanzisha uchunguzi tukio hilo.

Huku hayo yakijiri, Polisi wanasaka genge lililompiga risasi na kumuua dereva wa lori kwenye barabara ya Thika, Nairobi katika kisa cha mauaji ya kinyama. Dereva huyo alikuwa akiendesha lori la kukusanya taka na alikuwa amesimama kwenye eneo la Utalii tunnel wakati mtu aliyekuwa amejihami kwa bunduki aina ya AK47 na ambaye alikuwa amebebwa kwenye gari dogo alipompiga risasi. 

Alimpiga dereva huyo risasi kichwani na kifuani na kumuua papo hapo. Wahudumu wengine sita kwenye lori hilo waliokuwa wakipakia taka hawakudhurika bali waliachwa na mshangao.  Gari la mshukiwa liliondoka kwa kasi mara baada ya tukio hilo, nia ya mauaji hayo bado haijabainika.

Wakati huo huo mhudumu wa bodaboda alipigwa risasi na kujeruhiwa kabla ya kuibiwa Shilingi 170,000 mtaani Kayole jijini Nairobi. 

Mwathiriwa alikuwa amepewa pesa hizo kutoka kwa duka moja eneo hilo kupeleka benki alipovamiwa na wanaume wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki mita chache kutoka benki alikokuwa akienda.  

Alipigwa risasi mguuni na mkononi na mtu mmoja kabla ya kunyakua pesa hizo na kuondoka kwa kasi katika tukio la saa moja jioni siku ya Alhamisi.  

Polisi wanasema bado hawajapata washukiwa na wanaamini walikuwa wamearifiwa kuhusu uwepo wa pesa hizo.