Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Gideon Mbuvi anayejulikana kama Mike Sonko, amewazawadi wachezaji wa Harambee Starlets baada ya ushindi wao.
Mwanasiasa huyo maarufu alisherehekea ushindi wa timu hiyo dhidi ya timu ya Cameroon kwa kuipa Sh250,000.
Kwenye mechi hiyo, Harambee Starlets waliizaba Cameroon mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti katika mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake (WAFCON).
Sonko alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliofika uwanjani kushabikia mechi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa X, Sonko, alishiriki picha za video wakisherehekea pamoja na wachezaji hao.
Katika video hiyo, mwanasiasa huyo mwenye utata anaonekana akibadilishana nambari za simu na mchezaji mmoja wa kike kisha akaendelea kutuma pesa.
Katika taarifa yake, aliwapongeza wachezaji hao kwa ushindi waliostahili na kuongeza kuwa kuja kwake katika mechi hiyo ni bahati iliyopelekea ushindi wao.
”Niliwaambia mimi sina swara kwa mara ya kwanza katika historia ya soka nchini. Timu yetu ya soka ya wasichana Harambee starlets imeishinda timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Cameroon kwa jumla ya mabao 4-3.” alichapisha.
Vile vile,alitoa wito kwa serikali ya Kitaifa kuwaunga wachezaji hao mkono wanapoendelea kujipanga katika mechi za hapo mbeleni.
Hili lilipelekea mashabiki wengine kummiminia sifa na kutoa maoni kuhusu mechi hiyo.
"Hii ni ishara nzuri sana. Sonko unafanya hili kutoka moyoni mwako. Sonkoreee uongezewe miaka na Mungu akubariki sana"
Harambee starlets sasa inatazamiwa kumenyana na Gabon au Botswana katika raundi ya pili ya mchujo ambayo inatazamiwa kufanyika kati ya Novemba 27 hadi Disemba 5.
Mshindi katika raundi hii atapata kufuzu moja kwa moja Kwa mashindano ya WAFCON ya 2024 yatakayo chezwa Morocco.