Ombi la pili limewasilishwa katika mahakama kuu ya Milimani likitaka kubatilisha notisi ya gazeti la serikali iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ikiongeza ya ada na tozo za hati za kusafiria, vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, ndoa na vifo.
Mlalamishi Fredrick Bikeri anasema uchapishaji wa notisi ya gazeti la serikali la tarehe 6 Novemba 2023 unakiuka vifungu kadhaa vya katiba.
Mlalamishi kupitia mawakili wake Shanice Maingi na Danstan Omari alisema kwamba atadhihirishia mahakamani kwamba waziri Kithure Kindiki alifanya kinyume cha sheria kwa kuchapisha notisi ya gazeti la serikali.
Walisema hakushirikisha umma kama inavyotakiwa kisheria kabla ya tozo na ada mpya kutangazwa. Walisema nyongeza ya ada kutoka Shilingi 100 hadi Shilingi 1000 ni ya kiwango cha juu na Wakenya wengi hawatamudu hasa vijana wanaohitimu kidato cha nne na ambao wanahitaji vitambulisho kutafuta Kazi na masomo ya juu.
Jaji Lawrence Mugambi aliagiza mlalamishi kuwasilisha ombi lake kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi.