Kampuni ya mawasiliano nchini Kenya, Safaricom imetoa tangazo muhimu kwa watumizi wote wa huduma za miaala ya pesa, M-Pesa.
Katika taarifa yao iliyochapishwa katika kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii, Safaricom walitoa makataa ya hadi Februari 5 kwa watumizi wa M-Pesa ambao laini zao za simu hazijasajiliwa kwamba hawatoweza kupata huduma za M-Pesa tena.
Katika taarifa yake, kampuni ya simu za mkononi hata hivyo ilisema kuwa wateja waliosajiliwa wataweza kutuma na kupokea pesa kutoka kwa watoa huduma mbalimbali wa simu kama vile Airtel na T-Kash.
"Kuanzia Februari 5, 2024, hutaweza tena kutuma pesa kutoka kwa M-Pesa kwa wateja ambao hawajasajiliwa wa kutuma pesa kwa simu," Safaricom ilisema.
Safaricom imewataka wale ambao hawajasajiliwa kufanya hivyo.
"Tunawahimiza wateja ambao hawajasajiliwa kwa huduma za pesa kwa njia ya simu wajisajili kwa kutembelea Duka la Safaricom au wakala wa M-Pesa wakiwa na hati zao za utambulisho."
Hata hivyo, baadhi ya watumizi wa mitandao ya kijamii walionyesha kushangazwa kwao wakiuliza iwapo huduma hizo zimekuwa zikifanyika kwa watumizi wenye laini zisizosajiliwa.
Itakumbukwa miaka miwili iliyopita, Safaricom na kampuni zingine zote zilitoa makataa ya muda kwa watu wote kuhakikisha kwamba laini zao zilikuwa zimesajiliwa kuambatana na matakwa ya mamlaka ya mawasiliano nchini CA.