Rais wa Uganda Yoweri Museveni Jumatatu alasiri aliwakutanisha viongozi wapinzajni wa Kenya rais William Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga nyumbani kwake Kisozi.
Picha za mahasimu hao wawili wa kisiasa ziliwaonyesha wakizungumza na kiongozi wa Uganda huku wakitembea na fimbo mkononi, ng’ombe wa Museveni maarufu Ankole wakichunga kwa nyuma.
Rais Ruto alirejelea mkutano wao akisema uliangazia maswala muhimu yanayoathiri Kenya na Uganda, kama vile nishati na petroli.
"Nilikuwa na furaha kukutana na Rais nyumbani kwake Kisozi nchini Uganda. Tulijadili masuala muhimu ambayo yanaathiri nchi zetu mbili kama vile nishati na petroli," Rais Ruto alisema.
"Kenya na Uganda zimejitolea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi zetu mbili."
Kwa mujibu wa Rais Ruto, uhusiano wa Kenya na Uganda ni sehemu ya mpango mkubwa zaidi utakaoleta mataifa yote saba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki karibu na kuunda Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Alisema wakati wa mkutano huo, azma ya Raila kugombea Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika pia ilijadiliwa.
Rais Museveni aliwakaribisha viongozi hao wawili katika sasisho kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, akisema kuwa majadiliano yao yalilenga masuala ya pande zote mbili ambayo nchi zote mbili zinakabiliana nazo.
"Nilifurahi kukutana na Rais Ruto na Rt. Mh. Odinga alasiri hii katika shamba langu huko Kisozi. Tulijadili maswala yenye maslahi kati ya nchi zetu mbili. Ninawakaribisha," Museveni alisema.