Aliyekuwa gavana wa Kitui Charity Ngilu amemtaka kiongozi wao wa Azimio Raila Odinga kutowaacha wapweke akiwa atapata wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika (AUC).
“Baba umepangaje, Umetupangiaje… Unajua naambiwa niepuke siasa hapa lakini sijui kama naweza kuepuka siasa. Na nadhani wengi wenu hamtauliza, lakini nimekuwa na baba katika siasa kwa miaka mingi, kwa hivyo nitauliza,” Ngilu alisema.
Ngilu ambaye alikuwa akihutubia kongamano la biashara na uwekezaji katika kaunti ya Homa Bay alisema kama baba, Raila anafaa kupanga watoto (upinzani) kabla ya kuondoka.
“ni lazima mtoto akitoka kwa mamake au baba akiacha watoto lazima awapange kwa hivyo nataka kukuuliza baba tupange vizuri, unajua ulitupanga in 2002 lazima utupange tena ili tujuwe tunasonga mbele aje?,” Ngilu aliongeza.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametangaza ari ya kuania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika na amekuwa katika harakati za kutafuta uungwaji mkono kutoka mataifa mbali mbali.
Azma ya Raila imepigwa jeki na rais William Ruto baada ya kutangaza kwamba serikali yake itafanya juu chini kumpigia debe Raila.
Ruto akihutubia wananchi katika Kaunti ya Homa Bay siku ya Jumanne alisema kwamba ushindi wa Raila utakuwa wa Kenya na kwamba aliahidi wakati wa kampeni zake kwamba ataleta taifa na wakenya wote pamoja.
Raila analenga kuchukuwa nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na aliyekuwa waziri mkuu wa Chad Moussa Faki ambaye muda wake wa kuhudumu unakaribia kukamilika mwaka ujao.