Bunge la Ghana limepitisha kwa kauli moja muswada tata wa kupinga mapenzi ya jinsia moja ambao unaamuru kifungo cha miaka 3 jela kwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kifungo cha miaka mitano kwa kuendeleza shughuli za LGBTQ+.
Sheria hiyo imekosolewa vikali kwa kukiuka haki za watu wachache wa jinsia moja nchini humo.
Ghana ni nchi ya hivi karibuni ya Afrika kutunga sheria ya kupinga mapenzi ya jinsi moja baada ya Uganda. Sheria hiyo mpya inatoa adhabu kali, hadi kifungo cha miaka 10, kwa kuchapisha nyenzo zinazolenga watoto na kupiga marufuku shughuli za ufadhili.
Pia inawahimiza raia wa Ghana kuripoti kwa polisi, wakati waandishi wa habari wanaweza kuwa hatarini ikiwa ripoti zinachukuliwa kuwa za kuunga mkono mapenzi ya jinsi moja na watu wa jamii ya LGBTQ +.
Mswada huo uliwasilishwa katika bunge la Ghana mnamo Agosti 2021 lakini ulikosolewa sana.
Wale wanaopinga sheria hiyo wanasema sheria hiyo itakiuka haki na uhuru wa watu wachache wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja.
Lakini wanaounga mkono mswada huo wanasema utasaidia kuhifadhi maadili ya familia ya Ghana. Sheria hiyo inaanza kutekelezwa baada ya rais Nana Akufo Addo kutia saini.