Polisi siku ya Jumatano, waliwakamata wanawake wawili wanaoshukiwa kuendesha ofisi wakihadaa wananchi kuwa ni mawakili katika eneo la Kasarani, Nairobi.
Wawili hao walikamatwa na maafisa wa upelelezi na maafisa wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) walipokuwa wakiendesha shughuli zao kutoka katika orofa moja karibu na kituo cha polisi cha Kasarani.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kujifanya na kughushi nyaraka za kisheria.
Timu ya LSK inayoongozwa na Stephen Mbugua ilisema mawakili bandia sasa wamebadilisha mbinu zao na kuamua kufanya kazi katika maeneo ya makazi.
"Nyaraka mbalimbali za miamala zilipatikana kutoka kwa wawili hao, ikiwa ni pamoja na uhamisho wa mali na wosia," Mbugua alisema.
Aliwaonya wananchi na wanataaluma wenzake wa taaluma ya sheria dhidi ya kuwaandikisha watu wasio na sifa za kufanya kazi za kisheria akisema wana hatari ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufutiwa usajili.