Mwanamume mmoja kutoka kaunti ya Pokot Magharibi amebaki katika hali ya kuchanganyikiwa asijue la kufanya baada ya mkewe kufa wiki tatu tu baada ya kujifungua mapacha watatu na kuwaacha mayatima.
Julius Teletum mwenye umri wa miaka 44 katika mahojiano ya kutia huruma na Nation, alisema kwamba hakuwa amejitayarisha kwa maisha ya kuwalea wanawe wachanga bila mama yao, na kifo chake kimemuacha katika hali ya kuchanganyikiwa.
Baba huyo ambaye amebaki na jumla ya watoto 9 sasa bila mama, akiwa ameketi kando ya kaburi bichi la mkewe, alisema kwamba mkewe alijifungua Februari 2 na kufa wiki tatu baadae, Februari 21.
Mkewe Mercy Chepkorir mwenye umri wa miaka 39 alizikwa wiki jana.
“Februari 15 alianza kujisikia vibaya, tulimchukua hospitalini na akarudi nyumbani lakini hali yake haikuimarika. Tulimrudisha tena hospitalini lakini tukampoteza,” Teletum aliiambia Nation.
Bila mama, Bwana Teletum amejikuta akiwanywesha wanawe maziwa ya dukani ambayo anasema ni ghali kando na kwamba hakuwahi fikiria angejipata katika hali hiyo.
“Maziwa ya watoto dukani ni ghali, sio maisha ambayo nilikuwa nimejiandaa kuyakabili. Lakini fikira zangu zilibadilika pindi Mercy alipoaga,” alisema.
Mwanamum huyo asiye na kibarua maalum ameomba msaada na majirani wake wanaomsaidia kaitka malezi ya watoto hao wamemsaidia kuanzisha nambari ya malipo ya paybill kwa ajili ya michango.
“Hili ni pigo kubwa Zaidi nimewahi patwa nalo. Uchungu huu ni wa kiwango kingine kabisa, haswa ninapokumbuka kwamba mapacha wangu 3 hawana mama yao. Imenilazimu kuwatafuta majirani na watu wema kunilindia watoto hawa, ni kibarua kigumu sana haswa nyakati za usiku. Wakati mwingine nakosa kupata mtu wa kunisaidia kuwanyamazisha,” alisema.