Takriban wiki tatu baada ya kumpoteza mwigizaji mkongwe John Okafor almaarufu Mr Ibu, tasnia ya filamu ya Nigeria inaomboleza tena kwani imempoteza nguli mwingine, Bw Amaechi Muonagor.
Bw Muonagor alithibitishwa kufariki siku ya Jumapili, Machi 24 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa figo kwa muda mrefu. Amefariki akiwa na umri wa miaka 62.
Vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti kuwa mwigizaji huyo wa vichekesho alikuwa kwenye matibabu ya dialysis kabla ya kifo chake. Alikuwa amepooza kwa sehemu kutokana na ugonjwa wa figo ambao umechukua maisha yake.
Kifo cha muigizaji huyo mkongwe kimekuja siku chache baada ya video kusambaa ambapo alionekana akiomba msaada wa kifedha kutoka kwa Wanigeria ili kumwezesha kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya upandikizaji wa figo.
Bw Muonagor, ambaye ni baba wa watoto wanne alikuwa ameruhusiwa kutoka hospitali hivi majuzi, huku akingoja kuchangisha pesa za matibabu yake zaidi nje ya nchi.
Wiki iliyopita, marehemu alijitokeza kuomba msaada wa kifedha baada ya afya yake kudorora.
Video iliyomuonyesha muigizaji huyo mkongwe akiwa dhaifu huku akiwa amelala kitandani aking’ang’ana kuomba msaada wa kifedha ili kupandikizwa figo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii katika siku chache zilizopita.
Katika video hiyo, alionekana akiwa amevimba usoni na bandeji kifuani huku akijaribu sana kueleza hali yake na kuomba msaada.
"Watu wa Igbo, nawasalimu nyote," Muonagor anasikika akisema kwa lugha ya Igbo kabla ya kushindwa kuzungumza zaidi.
Baada ya kushindwa kuendelea kuzungumza, muigizaji mwingine, Kingsley Orji alionekana kuchukua nafasi akieleza kuwa msanii huyo mkongwe anasumbuliwa na matatizo ya figo.
"Haijakuwa rahisi. Amekuwa katika hali hii kwa miezi sasa, Anataka kwenda kupandikizwa figo," muigizaji Orji alieleza.
Aliendelea, "Amerudi kutoka ICU, siku kadhaa zilizopita. Alikuwa akipokea matibabu lakini sio vizuri. Tuliamua kumrudisha nyumbani kwa sababu hakukuwa na pesa lakini haifai, anazungumza vizuri. Tafadhali, anahitaji msaada wako.”
Muigizaji mwingine, aliyeketi karibu naye, anaendelea kulezea kwamba Muonagor anahitaji pesa kulipia upandikizaji wa figo nchini India.
Habari kuhusu kifo cha Bw Muonagor zinajiri wiki chache tu baada ya kifo cha muigizaji mwenzake mkongwe John Okafor almaarufu Mr Ibu.
Mr Ibu alifariki kutokana na mshtuko wa moyo mnamo Machi 2, 2024.
Mchekeshaji huyo alikata roho katika Hospitali ya Evercare nchini Nigeria, akiripotiwa kufariki dunia akiwa katika hali ya kukosa fahamu.