Papa Francis ametuma ujumbe wa kuwafariji Wakenya wakati nchi ikikabiliwa na mafuriko makubwa.
Katika ujumbe wake wa siku ya Jumatano, 1 Mei 2024, Papa alitoa wito wa kuiombea nchi ya Kenya wakati wananchi wanakabiliana na makali ya mafuriko.
Alisema kwamba yeye binafsi anawaombea Wakenya ambao wanakabiliwa na athari za mafuriko ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya takriban watu 200.
"Niko karibu kiroho na watu wa Kenya wakati huu ambapo mafuriko makubwa yamegharimu maisha ya watu wengi na kuharibu maeneo makubwa. Tuwaombee kwa pamoja wale wote wanaopatwa na maafa haya ya janga," Papa alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa X.
Haya yanajiri kufuatia mafuriko yanayoendelea nchini ambayo yamesababisha uharibifu wa maisha na mali.
Jumatano asubuhi, wakaazi wa Kitengela walikumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha katika jiji hilo na viunga vyake.
Wengi wao walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuomba usaidizi huku mashirika ya kibinadamu kama vile Msalaba Mwekundu wa Kenya yakichukua hatua ya kuzihamisha familia.
Wakaazi kadhaa hawakuweza kutoka nje ya nyumba zao mapema saa mbili asubuhi Jumatano kwa sababu ya hali ya mafuriko.
Taarifa za hivi punde kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya zinaonyesha kuwa angalau watu 11, sita kati yao wakiwa katika hali mbaya, walikuwa wamehamishwa.
Siku ya Jumanne, Rais William Ruto alitangaza kuwa mafuriko hayo yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 170.
Ruto na Baraza lake la Mawaziri walikutana asubuhi hiyo na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mvua hiyo ambayo, kando na kupoteza maisha, imeharibu mali na maisha ya Wakenya wengi.
Idara ya utabiri wa hali ya anga ilisema Kenya itaendelea kupokea mvua zilizoimarishwa katika wiki zijazo, na kusababisha matatizo zaidi kwa familia ambazo tayari zimehama.