Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki ameamuru watu wanaoishi katika maeneo yaliyokaribu na mabwawa 178 kote nchini kuhama mara moja.
Serikali imewapa wakazi hao hadi saa 12.30 jioni Ijumaa, Mei 3, 2024, kuondoka au waondolewe kwa nguvu.
Maagizo ya serikali pia yanalenga watu wote wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi na matope, pamoja na wale wanaoishi ndani ya vitongoji vya karibu vya mabwawa 178 ya umma na ya kibinafsi ambayo yanakaribia au tayari yamejaa.
Maagizo ya kuhama yanajiri wakati watu ambao huenda wakaathiriwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi kutaka serikali kuwapa maeneo mbadala ya kuhamia.
Serikali imewahakikishia watu walioathirika kuwa makazi ya muda, pamoja na chakula na vifaa muhimu, vitatolewa ili kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu.
Zaidi ya hayo, mchakato wa uhamishaji utafanywa kati ya saa 12:00 asubuhi na 12:30 jioni ili kuhakikisha usalama wa wakaazi na maafisa wanaondesha zoezi la kuwahamisha.
Maafisa wa Utawala wa Serikali wameagizwa kushirikiana kwa karibu na serikali za kaunti, mashirika ya misaada ya kibinadamu, na washikadau wengine ili kuwezesha shughuli ya kuwahamisha watu kwa wakati na kwa njia ya kiutu.
Maagizo hayo pia yanawahusu watu wanaoishi ndani ya ukanda wa mito wa mita 30 na mikondo mingine ya maji kote nchini. Pia wameagizwa kuondoka mara moja kwa ajili ya usalama wao, huku makazi haramu katika maeneo haya ya pembezoni yakiondolewa.