logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mgao wa ruzuku ya mbolea kupunguzwa hadi Shs. bilioni 10

Kiasi kimepunguka kwa asilimia 38.2 kutoka bilioni 16.2 mwaka wa 2023/24.

image
na Davis Ojiambo

Habari13 June 2024 - 14:55

Muhtasari


  • • Mbolea inacheza jukumu kubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kiwango cha ndani.
    •Kupunguzwa kwa bajeti kunakuja wakati ambapo programu imekuwa suala tete
Waziri wa Hazina Njuguna Ndung'u

Katibu wa Hazina Njuguna Ndung'u amependekeza kutengwa kwa shilingi bilioni 10 kwa mpango wa ruzuku ya mbolea katika mwaka wa fedha ujao.

Kiasi hicho kimepunguka mno kwa asilimia 38.2 kutoka shilingi bilioni 16.2 ambazo hazina iliwekeza kwa mradi huo katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24.

Hapo awali, kiwango hiki kilikuwa shilingi bilioni 12.2 wakati bajeti ilipopitishwa Juni 2023 ila kiliongezwa kupitia bajeti ya marekebisho ambayo iliongeza shilingi bilioni 4.

Kupitia ruzuku hiyo, wakulima waliosajiliwa hulipa shilingi 2,500 kwa mfuko wa kilo 50 ya mbolea, ambayo ni pungufu kubwa ikilinganishwa na bei sokoni ambayo inaweza kufikia shilingi 6,500.

Mbolea ina jukumu kubwa katika kuongeza uzalishaji wa chakula nchini kwani ukulima ndio uti wa mgongo wa taifa.

Kupunguzwa kwa bajeti kunatokea wakati programu hiyo imekuwa suala tete baada ya kubainika kuwa wakulima walikuwa wanauziwa mbolea ghushi ambayo ilisababisha upotezaji wa mabilioni ya hela za walipa kodi.

Akitoa mukhtasari wa matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25, Ndung’u alisema serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 54.6 kwa ajili ya mageuzi ya kilimo na ukuaji jumuishi.

Katibu huyo alisema fedha hizo zitaelekezwa kwenye programu mbalimbali chini ya sekta kubwa ya kilimo katika kipindi cha matumizi kuanzia Julai 1.

Serikali imetenga shilingi bilioni 6.1 kwa programu ya maendeleo ya mlolongo wa thamani wa kilimo kitaifa.

Wakati huo huo, shilingi bilioni 2.5 zimetengwa kwa Programu ya Wezesha Vijana chini ya sekta ya kilimo na shilingi bilioni 2.4 kwa Mradi wa Wezesha Vijana na Wanawake katika Kilimo.

Serikali pia imetenga shilingi milioni 747 kwa mlolongo wa thamani wa umwagiliaji wa kibiashara na shilingi milioni 645 kwa mradi wa usalama wa chakula na upandaji wa mazao mbadala.

Kwa lengo la kuboresha uzalishaji wa mifugo, Ndung’u alipendekeza kutengwa kwa shilingi bilioni 2.4 kwa mpango wa kupunguza hatari katika mifumo ya uchumi wa kipastori na shilingi bilioni 1.1 kwa mradi wa mlolongo wa thamani wa mifugo.

Shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa programu ya biashara ya mifugo huku shilingi milioni 195 kwa mradi wa uhamishaji wa viini na shilingi milioni 300 kwa maendeleo ya viwanja vya viwanda.

"Serikali itaendelea kuwa na mkazo katika mageuzi ya kilimo na ukuaji jumuishi kupitia msaada wa mlolongo wa thamani," alisema Ndung'u.

"Hii inakusudia kusaidia wakulima kupitia vyama vya ushirika ambavyo tunaviona kama wakusanyaji na kutumia vyombo vya kisasa vya usimamizi wa hatari ambavyo vinahakikisha kilimo kinakuwa cha faida na bei zinatabirika."

Ndung'u alisema bajeti hizo zinalenga kuhamisha wakulima kutoka kwenye upungufu wa chakula hadi kuwa wazalishaji wa ziada kupitia ufadhili wa pembejeo, ruzuku, na huduma za ugani wa kilimo.

Bajeti ya 2024/2025 inakadiriwa kugharimu takriban shilingi trilioni 3.91.

Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 1.58 imelengwa kwa matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 727.9 kwa matumizi ya maendeleo, shilingi trilioni 1.21 kwa huduma za mfuko wa pamoja na shilingi bilioni 400 kwa mgao wa haki kwa kaunti.

Kwa ajili ya kufadhili bajeti hii, serikali inalenga kukusanya shilingi trilioni 2.91 kutoka kwa mapato ya kawaida na shilingi bilioni 441 kutoka kwa makadirio ya wizara kwa msaada.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved