logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Binti wa rais wa Cameroon adokeza kuhusu uhusiano wa watu wa jinsia moja

Pia alishirikisha ujumbe mwingine kutoka kwa watu wakionyesha kumuunga mkono.

image

Habari04 July 2024 - 12:00

Muhtasari


  • Picha hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa Instagram inaonyesha Brenda Biya mwenye umri wa miaka 26 akimkumbatia mwanamitindo wa Brazil Layyons Valença.

Binti wa rais wa Cameroon amesambaza picha akiwa anambusu mwanamke mwingine, jambo ambalo limezua hisia tofauti katika nchi ambayo mahusiano ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha sheria.

Picha hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa Instagram inaonyesha Brenda Biya mwenye umri wa miaka 26 akimkumbatia mwanamitindo wa Brazil Layyons Valença.

"Ninakupenda kupita maelezo na ninataka ulimwengu ujue," Biya aliandika, akiongeza emoji ya mapenzi.

Baba yake mwenye umri wa miaka 91, Paul Biya, alikua rais wa Cameroon mwaka 1982 na ni mmoja wa viongozi waliotawala kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Wale wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja au mahusiano ya aina hiyo katika taifa hilo la Afrika ya Kati wanakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela.

Bi Biya - mwanamuziki anayeishi ng'ambo anayejulikana kwa jina la King Nasty - hakutaja wazi jinsia yake alipochapisha picha ya busu hilo.

Hata hivyo, muda baada ya picha hiyo kuchapishwa, Bi Biya alishirikisha makala kutoka Le Monde, ambapo gazeti la Ufaransa liliripoti kwamba "amejitokeza".

Pia alishirikisha ujumbe mwingine kutoka kwa watu wakionyesha kumuunga mkono.

Mwanaharakati wa Cameroon aliyebadili jinsia, Shakiro alikuwa miongoni mwa waliomsifu Biya, akisema ujumbe wake wa Instagram unaweza kuwa "mabadiliko kwa jumuiya ya LGBTQ+ nchini Cameroon".

Shakiro alisema Bi Biya "sasa anajiweka kama sauti ya mabadiliko ya kijamii katika nchi ambayo miiko imekita mizizi".

Kwa sasa Shakiro anaishi Ubelgiji. Alitafuta hifadhi huko baada ya kuhukumiwa kwa "jaribio la mapenzi ya jinsia moja" nchini Cameroon.

Ingawa Biya amesifiwa na watu wengine, watumiaji kadhaa wa mitandao ya kijamii nchini Cameroon walijibu ujumbe wake kwa maoni ya chuki dhidi ya mapenzi ya jinsia moja.

Baadhi wameuliza ikiwa Bi Biya alishirikisha picha hiyo ili kuzua gumzo, ikizingatiwa sifa yake ya kuweka ujumbe kwenye mitandao ya kijamii ambao huzua mijadala miongoni mwa raia wa Cameroon.

 

 

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved