Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Nairobi Esther Muthoni Passaris amefichua kuwa hivi majuzi alifanyiwa upasuaji.
Mwanasiasa huyo alifichua hayo alipokuwa akimjibu mtumiaji wa Twitter ambaye aliuliza jinsi anavyoendea.
Passaris alisema kuwa anahisi uchovu kwani alifanyiwa upasuaji wiki mbili zilizopita na akashauriwa kuchukua mapumziko ya wiki tatu, ushauri ambao hakuuchukua.
"Nahisi uchovu. Ni wiki mbili tangu upasuaji wangu. Nilipaswa kutii ushauri wa madaktari wa kuchukua mapumziko ya kitanda cha wiki tatu lakini wajibu uliniita na nina shauku ya kutumikia. Ninafanya kila niwezalo na najua Mungu ananipenda kwa vile nilivyo na ninachofanya. Mimi ni mwanamke anayeufuata moyo wa Mungu mwenyewe,” Passaris alijibu.
Mwanasiasa huyo wa ODM aliendelea kuwahutunbia wakosoaji wake akisema hawana ufahamu mzuri.
“Mengine yote hayana maana; Ninaweza tu kuwaombea wanaochukia kwa sababu hawajui zaidi. Wamejawa na hukumu na wanajiona watakatifu kuliko mtazamo wako. Ninawatumia upendo na amani kwa sababu hawajui zaidi. Asante kwa kuuliza. Tutaongea kesho. Usiku mwema, watu wema," aliongeza.
Shughuli ya hivi majuzi haikuwa mara ya kwanza kwa Passaris kufanyiwa upasuaji, amefanyiwa upasuaji mara zingine kadhaa siku za nyuma.
Mnamo Januari 2020, Mwakilishi huyo wa Kike wa Nairobi alifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo katika Hospitali ya CIMS nchini India.
Katika taarifa, Passaris alisema kuwa alifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo Januari 1, siku moja baada ya kusafiri kuelekea India.
Mwanasiasa huyo alichapisha video kupitia ukurasa wake wa Twitter akitembea kwa magongo huku akipata uthabiti baada ya upasuaji.
Aliongeza kuwa alikuwa akihangaika kupata nafasi nzuri ya kulala na ilikuwa inamlazimu kurekebisha mkao wake wa kulala.
Passaris alikuwa amefanyiwa upasuaji mwingine katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi mnamo Septemba 2019 baada ya kuwa na tatizo la mgongo wake.
Mwanasiasa huyo alikuwa amesema kwamba amekuwa na tatizo la mgongo wake kwa karibu miongo miwili.
Alisema kuwa ameshauriana na zaidi ya madaktari kumi nchini kuhusu hali yake.