Rais William Ruto alikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa michezo wa Talanta,jijini Nairobi.
Kwenye ziara yake ,Jumanne alasiri rais alisema kuwa uwanja huo wa michezo utakamilika kabla ya mwisho wa mwaka ujao tayari kuandaa kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) mnamo 2027.
“Nimekuja hapa leo kukagua maendeleo ya kazi za ujenzi wa uwanja huu. Tutaajiri watu wengi zaidi ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kabla ya mwisho wa mwaka ujao,” Rais alisema.
Uwanja huo unatazamiwa kutumika kwenye mechi mbali mbali za Afcon 2027.
Rais pia alisema kuwa mradi huo utafafanua upya wasifu wa michezo wa Kenya na kusababisha kituo cha kipekee na uboreshaji wa miundombinu kwa jiji la Nairobi na taifa.
Alibainisha kuwa Kenya ina nia ya kuendeleza na kutekeleza mpango kabambe wa miundombinu ya sekta ya michezo na ubunifu.
Alisema serikali inaboresha miundombinu mbalimbali ya michezo ili kutoa mafunzo bora kwa wanamichezo na wakati huo huo, kukuza vipaji vya michezo nchini kote.
Muundo uliozinduliwa na serikali miezi michache iliyopita unaonyesha kituo hicho kitakuwa na vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya timu na wasimamizi wa mechi.
Pia kutakuwa na utoaji wa vyumba vya matibabu, chumba cha kudhibiti vipimo vya wachezaji na maeneo yanayohusiana na watazamaji, sehemu ya watu mashuhuri, sehemu ya vyombo vya habari, na maeneo mengi ya utangazaji. Zaidi ya hayo, serikali itajenga miundombinu ya ICT na maeneo ya maegesho.
Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) linataka uso wa uwanja uwe wa kijani kibichi, usawa, na uwekwe alama nyeupe. Alama kwenye uwanja zinapaswa kuwa linganifu katika uwanja wote wa mchezo.
Kabla ya hapo, Rais Ruto alikuwa ametembelea shule ya msingi ya Lenana, ambako madarasa zaidi yanajengwa ili kukidhi ongezeko la wanafunzi katika taasisi hiyo.