Ukisema ni "Ndege wavamizi wa ajabu " huenda ikasikika kama filamu ya kufikirika na ya kutisha ya Hollywood, lakini kwa wakazi wa pwani ya kenya sio jambo la kufikirika.
Maafisa wa pwani ya Kenya wana wasiwasi mkubwa juu ya kero inayoletwa na kunguru hao ambao asili yao ni India kiasi kwamba sasa wameanza harakati za kuwaua milioni moja.
Ndege hawa huwalenga wanadamu, kama katika filamu ya kutisha ya Alfred Hitchock The Birds, lakini hawa kwa miongo kadhaa wamesababisha usumbufu mkubwa, kwa kuwinda wanyamapori, kuvamia maeneo ya kitalii na kushambulia vibanda vya kuku.
Sumu sasa inatumika katika miji ya Watamu na Malindi kuua kundi la kwanza la spishi hii ndogo katili.
Kampeni hii kabambe ya kutega sumu inalenga kuwakomesha kunguru kuelekea mji mkuu, Nairobi.
Ndege hao, wanaojulikana pwani kama "kunguru" au "kurabu", walitoka India na sehemu nyingine za Asia, na mara wamekuwa wakihamia mara kwa mara mahali pengine kwa kutumia usafiri wa meli za biashara.
Lakini inaaminika kuwa waliletwa kimakusudi katika Afrika Mashariki karibu miaka ya 1890 katika jitihada za kukabiliana na tatizo la taka lililokuwa likiongezeka katika visiwa vya Zanzibar, ambavyo wakati huo vilikuwa chini ya ulinzi wa Uingereza. Kutoka huko, walienea hadi bara na kupanda pwani hadi Kenya.