logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mahakama yaharamisha polisi kufunika nyuso wakati wa maandamano

LSK iliambia mahakama kutumwa kwa maafisa waliovalia mavazi ya kiraia kunaleta hali ya sintofahamu

image
na Davis Ojiambo

Habari15 August 2024 - 04:23

Muhtasari


  • • IG anapaswa kuhakikisha kuwa maafisa wake hawafichi kitambulisho au usajili wa gari lolote linalotumiwa wakati wa kushughulika na watu wanaoandamana.

Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya ameagizwa kuhakikisha kuwa maafisa waliovalia kiraia hawafuniki nyuso zao wanapokabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano.

Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alisema Inspekta Jenerali anapaswa kuhakikisha zaidi kuwa maafisa wake hawafichi kitambulisho au usajili wa gari lolote linalotumiwa wakati wa kushughulika na watu wanaoandamana.

Jaji alitoa maagizo hayo kufuatia ombi lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini Kenya LSK.

LSK kupitia kwa wakili Dudley Ochiel iliambia mahakama kutumwa kwa maafisa waliovalia mavazi ya kiraia kila mara kunaleta hali ya sintofahamu ambayo hatimaye inazuia haki ya watu kuandamana.

"Maafisa hawa ambao hawajatambuliwa hawawezi kuwajibika kwa matendo yao. Matokeo yake wanaishia kutumia nguvu kupita kiasi. Hawawezi kuwajibika kwa sababu hawajulikani," alisema Ochiel.

Alimwambia Jaji kwamba isipokuwa mahakama kuingilia kati na mwelekeo huo kukomeshwa, Wakenya wana hatari ya kifo na kunyimwa haki zao kwa mujibu wa katiba.

Jaji Bahati ambaye aliidhinisha suala la LSK kuwa la dharura aliagiza IG kuhakikisha kuwa kuna utiifu kamili katika suala la kuhakikisha kwamba maafisa wote waliovalia sare wataweka majina yao katika sare walizovalia kila wakati au nambari ya huduma inayotambulika.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved