Idara
ya mahakama ya Kenya kwa mara nyingine imetumbukia katika hali ya majonzi kufuatia
kifo cha hakimu Mh. Bernard Kipyegon Rugut.
Habari
za kifo cha Rugut zilithibitishwa na Jaji Mkuu Martha Koome Jumanne asubuhi ambapo
alimuomboleza kwa niaba ya Idara ya Mahakama.
Marehemu
alikuwa hakimu mkuu katika Mahakama ya Sheria ya Molo hadi wakati wa kifo
chake.
“Kwa
masikitiko makubwa na moyo mzito natangaza kifo cha Mhe. Bernard Kipyegon
Rugut, Hakimu Mkuu katika Mahakama za Sheria za Molo,” Koome alitangaza katika
taarifa yake.
“Kwa
niaba ya Mahakama, napenda kumpa pole mke wake, Mhe. Purity Koskey Rugut wa
Mahakama ya Sheria ya Kabarnet, watoto wao, familia nzima, jamaa, marafiki, na
wafanyakazi wenzake wa Mhe. Rugut wakati huu mgumu sana, "aliongeza.
Kulingana na Jaji Mkuu, Rugut alianza taaluma yake na mahakama mnamo Julai 13, 2012 alipoteuliwa kuwa hakimu mkazi na kutumwa katika Mahakama za Sheria za Bondo.
"Kwa miaka mingi, alihudumu kwa kujitolea thabiti katika vituo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Sheria ya Ndiwa na Kericho, akionyesha kujitolea kwa dhati kwa kanuni za haki. Hivi majuzi, tangu Mei 2, 2023, alihudumu kama Hakimu Mkuu katika Mahakama za Sheria za Molo,” Koome alisema.
Jaji mkuu aliendelea kumtambua marehemu Rugut kwa bidii yake, haki na weledi wake katika majukumu yake yote ya mahakama.
"Kuaga kwake sio tu hasara kubwa kwa familia yake lakini pia kwa Mahakama na jamii alizotumikia kwa uaminifu. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na wapendwa wake tunapoomboleza kifo cha afisa wa mahakama aliyejitolea ambaye urithi wake wa utumishi unaendelea kututia moyo sisi sote. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele,” Koome alisema.